Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena Bwana ametupa ili tuendelee kumtukuza na kumzalia matunda yaliyo mema.
Siku kama ya leo wengi wetu tunaenda kanisani, hata yule ambaye hajaonekana siku za katikati ya wiki. Leo atajitahidi afike ibadani kwa ajili ya Bwana.
Pamoja na wengi wetu kuingia ibadani/kanisani, wengi wetu huwa tunaingia tukiwa hatuna maandalizi ya kutosha ndani mwetu.
Maandalizi ninayoyazungumza hapa, ni maandalizi ya *MOYO WAKO* moyo wako una weza kukutanisha na Mungu wako, moyo wako unaweza kukutanisha na jibu la ombi lako, na moyo wako unaweza kuzuia kupokea jibu lako.
Utasema kwanini moyo na si kitu kingine, moyo wako ndimo palipo na kila kitu, akili yako imo moyoni, mawazo yako mazuri/mabaya yamo moyoni mwako.
Hebu turejee andiko hili katika biblia;
Mipango ya moyoni ni ya mwanadamu, bali jibu la ulimi hutoka kwa Bwana .Mithali 16:1. NEN.
Katika biblia ya NENO imeeleza vizuri mipango ya moyoni ni ya kwako wewe, ila jibu la lile uliloliomba na lile ambalo hukiliomba utalipata kwa maandalizi ya moyo wako kuwa tayari kupokea kitu kutoka kwa Bwana.
Labda niseme hivi unaweza kunielewa; kujiandaa kusikiliza ujumbe si kutaka tu mtoa ujumbe aeleze kile umeomba kwa Mungu, kusikiliza kunakupa kupokea kitu kitakachokusaidia maishani mwako.Katika kusikiliza unakutakana na jawabu/jibu la Mungu kwa lile ambalo huenda uliomba miaka mingi.
Kujiandaa kusikia pia kunakupa nafasi zaidi ya kumsikia Mungu akisema na wewe maeneo mbalimbali ya maisha yako, yapo maonyo utapewa, yapo maagizo utapewa, na yapo maeneo utafunguliwa na kuondolewa utata.
Kushindwa kwako kujua kama umejibiwa ni kukosa maandalizi ya moyo wako, wakati mwingine majibu yako yameshindwa kukufikia kwa kukosa maandalizi.
Huenda umekuwa na kiu ya kukutana na nguvu za Roho Mtakatifu, huenda umetamani kunena kwa lugha mpya. Badala yake umebaki kushuhudia wengine wakinena kwa lugha mpya, umebakia kushangaa. Fahamu kwamba unapaswa kufanya maandilizi ya ndani ya moyo wako.
Mungu hajashindwa, bali anakuhitaji wewe utengeneze maandilizi ya kukutana naye. Unaweza kulalamika mtumishi wa leo amekuvuruga kumbe ulienda ibadani kwa kukurupuka.
Utakuta mtu upo ndani ya ibada lakini mawazo yako yote yapo nyumbani, kazini, shuleni, chuoni, na mawazo mengine yapo kwa mtu aliyekukosea.
Unakuwa ibadani lakini wewe wa ndani upo nje, ila mwili wako upo ndani ya hekalu. Tunakuona umekaa kwenye kiti kumbe unagombana na jirani/wafanyakazi/boss/mwalimu/mke/mume wako ambaye hata hayupo hapo ulipo.
Naona nimekuchanganya, ipo hivi; hujawahi kujikuta upo sehem na watu wanaongea sana lakini anatokeza mtu kati yenu anakushtua na kukuambia we vipi mbona unaonekana upo mbali sana kimawazo! Utashtuka na kuzinduka, na kurudi Katika hali yako ya kawaida.
Mpaka hapo utakuwa umenielewa, ndio maana NENO LA MUNGU linasema; *Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa BWANA. MIT. 16:1. SUV.*
Hakikisha unaingia ibadani na maandalizi ya moyo wako, hakikisha mawazo yako yote unayeweka ibadani, acha kwanza hayo mawazo mengine nje. Jitahidi kurudisha moyo wako ibadani, achana na madeni yako, Mungu atakupa akili ya namna ya kuwalipa wanaokudai.
Usiache kukusanyika pamoja.
Samson Ernest.
+255759808081.