
Mambo mengi yanayowapata watu wengi leo, ni yale matokeo ya yale waliyoyapanda huko nyuma, kama mtu alipanda wema, upo wakati atavuna matunda ya wema wake. Na kama alipanda ubaya, upo wakati utafika atavuna matunda ya ubaya wake.
Unayemwona leo Mungu amemwinua kwenye huduma yake, haijatokea ghafla huyo mtu akawa hapo juu, ipo gharama kubwa imetoka kabla hajafika kiwango alichofikia. Uvumilivu wake na kuendelea kuishi maisha matakatifu, ndicho kilichomfikisha hapo alipo.
Wakati mwingine alionekana mtu asiye na kitu cha kuwabariki wengine ila inapofika wakati wa Bwana, wengi sana humfurahia, na wengine hugeuka na kuonekana walikuwa wanajua atafika hapo alipo. Na wakati walikuwa wanampuuza, ama walikuwa sehemu ya kumvunja moyo.
Yapo mapando mengi sana ambayo watu huwa wanapanda katika maisha yao, na mapando hayo wengi wetu huwa hatuyakumbuki pale yanapoanza kuzaa matunda yake. Hasa matunda yakiwa mabaya, huwa tunaona imetokea ghafla, kumbe ni mambo ya siku nyingi tuliyofanya.
Mbaya zaidi tulifanya mabaya, au tuliwafanyia wengine mabaya, alafu hatukubu kwa Mungu wetu, tukawa tumeendelea na maisha yetu ya kuwaumiza wengine, au tukawa tumepumzika.
Siku tusiyoijua/tusiyoitarajia katika maisha yetu, yale mabaya yote tuliyokuwa tunawafanyia wengine, yatageuka kwetu kwa namna ambayo hatukuijua. Kumbe wakati ambao tulikuwa hatujapatwa na hayo, Mungu alitupa muda tutubu.
Mungu anapofika hatua ya kutuadhibu sio mara zote tufikirie kwa namna mbaya, wakati mwingine ni njia ya kutumbusha tunapaswa kumrudia yeye kwa kutubu. Na kuanza upya na yeye.
Usijidanganye hayo mabaya unayoyatenda yataishia tu hewani, haijalishi yatachukua muda gani, uwe na uhakika utavuna matunda ya kazi yako ya ubaya ulioutenda.
Rejea: Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. GAL. 6:7 SUV.
Hapa nimezungumzia sana kwa upande wa ubaya, ila upo upande mwingine wa mazuri, unaweza kutenda mema sana. Wakati mwingine usione matokeo mazuri ya wema wako, nakuhakikishia upo wakati utavuna matunda ya wema wako.
Kama unafanya wema huo kwa utukufu wa Bwana, alafu unapokea matokeo mabaya, uwe na uhakika hayo hayawezi kuzuia saa yako ya kuja kuvuna matunda ya wema wako.
Andiko takatifu lipo wazi kwa hili, usifikiri ni utani, usipozimia moyo wako katika kutenda mema, uwe na uhakika utavuna kwa wakati wake. Tena wakati wa Mungu huwa sahihi siku zote, japo kibinadamu huwa tunaona tofauti, ndio maana unapaswa kusoma Neno la Mungu.
Rejea: Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. GAL. 6:9 SUV.
Je, umeacha kutenda mema kwa sababu umevuna matokeo mabaya ya wema wako? Maandiko yanatusihi “TUSIZIMIE MIOYO” yetu. Tuendelee kutenda mema, tutavuna kwa wakati wake Mungu mwenyewe.
Soma Neno la Mungu(Biblia) uendelee kufahamu mambo mbalimbali ya kukusaidia katika maisha yako ya wokovu, bila Neno la Mungu utajikuta ni mtu usiye na mwelekeo sahihi.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com