“Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia”, Mt 3:2 SUV.

Toba maana yake ni “kugeuka”, kugeuka kutoka katika njia mbaya za uovu na kumgeukia Yesu Kristo, na kwa kupitia yeye, unamgeukia Mungu (Yn 14:1, 6; Mdo 8:22, 26:18).

Uamuzi wa kugeuka kutoka katika dhambi na kugeukia wokovu katika Kristo, unahusisha kumpokea Kristo si tu kama Mwokozi kutoka katika adhabu ya dhambi, bali pia kama Bwana wa maisha ya mtu au maisha yako.

Hivyo, toba inahusisha kubadilisha mabwana wawili, yaani kutoka katika ubwana wa Shetani (Efe 2:2) na kwenda katika ubwana wa Kristo na Neno lake (Mdo 26:18).

Toba ni uamuzi huru kwa upande wa wenye dhambi, unaofanikishwa na neema iwezeshayo ambayo watu hupewa wanaposikia na kuiamini Injili ya Yesu Kristo.

“Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana”, Mdo 11:21 SUV.

Kutoa maana ya Imani iokoayo kuwa ni kumwamini tu Kristo kama Mwokozi hakutoshelezi kabisa kutokana na madai ya Kristo kuhusiana na toba.

Kutoa maana ya Imani iokoayo katika njia ambayo siyo lazima ihusishe kuachana kabisa na dhambi ni kuharibu vibaya sana mtazamo wa Kibiblia wa ukombozi.

Imani inayohusisha toba mara zote ni sharti la wokovu;

“Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu”, Mdo 2:38 SUV.

Toba ilikuwa ni ujumbe wa msingi wa manabii wa Agano la Kale (Mal 3:7; Eze 18:30; Yer 7:3), Yohana Mbatizaji (Mt 3:2), Yesu Kristo (Mt 4:17) na Wakristo wa Agano Jipya (Mdo 2:38; Lk 5:32).

Kuhubiri toba ni lazima kuende sanjari au sambasamba na ujumbe wa Injili (Lk 24:47), tofauti na hapo ujumbe wa injili bado haijakamilika.

Unaposikia unaambiwa tubu na uache dhambi zako ufalme wa Mungu umekaribia usifikiri ni jambo ambalo haliwezi kutokea, unaweza ukajifariji kuwa hizi habari nimeanza kuzisikia siku nyingi sana na sikuona lililotokea, kwanza mshukuru Mungu kukupa uhai hadi sasa na unasoma Makala hii.

Yesu anakuita utoke kwenye maisha ya dhambi uje kwake, utubu dhambi zako zote, utoke katika miliki ya Shetani na kuja kwenye miliki yake, inakuhitaji wewe kuchukua hatua. Usipochukua hatua utaelendelea kuwa mfuasi wake na siku ya mwisho utatupwa jenahamu ya milele pamoja naye.

Na wewe ambaye ulirudi nyuma, yaani ulirudi kumilikiwa na Shetani, unapaswa kutoka huko na kurudi kwa Yesu Kristo, Imani zingine zinaweza kukudanganya upo salama na huna shida Yesu alishakuokoa, hiyo Imani siyo sawa, unapaswa kumrudia Mungu wako na kuacha matendo mabaya.

Yesu yupo tayari kukupokea na kukufanya mtu mpya kabisa katika Kristo, hata ukifa leo unayo matumaini ya kufufuliwa na kuketi pamoja na Bwana Yesu. Amua sasa kumfuata Yesu, uwe salama.

Mwisho, jiunge na group la wasap la kusoma biblia kila siku kwa kufuata mtiririko mzuri, wasiliana nasi kwa wasap namba +255759808081.

Soma neno ukue kiroho

Mungu akubariki sana

Samson Ernest

+255759808081