Tunapokuwa tumejitenga na mabaya ya dunia hii usifikiri tumemfurahisha shetani, na usifikiri ataacha kutufuatilia.

Unapokuwa na huduma nzuri yenye kusaidia na kugusa maisha ya watu, kwa kuwaondoa kwenye vifungo mbalimbali vya mwovu shetani kwa kulitangaza jina la Yesu. Usifikiri kitendo kile kinamfurahisha sana baba wa maovu.

Unaweza kufikiri marafiki/ndugu wanakutakia mema kila mmoja wao kwa nafasi uliyonayo ya utumishi wa Mungu.

Tunaona habari hizi kwa mfalme Daudi, wakati Daudi amekaa kwenye nafasi ya ufalme, huku nyuma Absalom alikuwa anapanga mashambulizi ya kumwondoa baba yake ili yeye achukue nafasi ya ufalme.

Rejea;

Nami nitamshambulia wakati atakaokuwa amechoka, na mikono yake imekuwa dhaifu, nami nitamtia hofu; na watu wote walio pamoja naye watakimbia; nami nitampiga mfalme peke yake;
na hao watu wote nitawarejeza kwako; mtu yule umtafutaye ni kana kwamba wamerudi wote; na hivyo watu wote watakuwa katika amani.
2 Samweli 17 :2_3.

Umeona hapo, unaweza kujiona huna tatizo na watu kumbe shetani anawatumia watu walewale kutaka kukuangamiza na kukutoa katika nafasi uliyonayo.

Pamoja na wengine wanapanga mabaya juu yako, Mungu ana watu wake wanapanga mema juu yako. Wapo tayari kukulinda kwa namna yeyote ile usimalizwe na adui maana Mungu anawatumia kukuepusha na hila mbaya.

Yesu ana mpango mwema na maisha yako, haijalishi adui amepanga mabaya juu yako, tunafahamu Mungu akiwa upande wetu hakuna aliye juu yetu.

Tunasoma wakati Absalom wanapanga na Athiofeli na kikundi chake kwenda kumshambulia Daudi, baada ya kuafikiana Absalom alitaka kusikia kwa Hushai anatoa maoni yake. Hushai alitoa ushauri wa kutofautiana na kundi la Athiofeli, nia yake ikiwa tofauti kabisa.

Kumbe ndani ya moyo wa Hushai Mungu aliweka upendo ili kumwepusha Daudi na hatari ambayo ilikuwa inapangwa na kundi lake kuondoa uhai wa mtu ambaye hakuwa na hatia, kwa lugha ya sasa tunaweza kusema Hushai amewasaliti wenzake kwa kutoa siri ya jeshi.

Rejea;

Ndipo Hushai akawaambia Sadoki na Abiathari, makuhani, Ahithofeli amempa Absalomu na wazee wa Israeli mashauri kadha wa kadha; na mimi nimetoa mashauri kadha wa kadha.
Basi sasa pelekeni habari upesi kamwambieni Daudi ya kwamba, Usilale usiku huu karibu na vivuko vya jangwani; bali usikose kuvuka; asije akamezwa mfalme, na watu wote walio pamoja naye. 2 Samweli 17 :15_16.

Nina uhakika umewahi kuona watu walikuwa wana kusema vibaya na kupanga mabaya ju yako. Anatokea mwenzao katika kundi lile kuja kukuambia roho yako inatafutwa ondoka upesi eneo hili, na mtu yule akitaka kuacha kuja kukupa taarifa anashangaa kelele haiondoki ndani yake mpaka ameleta taarifa.

Anaweza kuona ni yeye kumbe ni Mungu amemsukuma kufanya vile, hahitaji wewe kufunuliwa wakati hatari ipo mbele yake masaa machache. Elewa wakati mwingine sio lazima Mungu afanye hivyo anachofanya ni kutuma mtu wake.

Mungu wetu ni mwema siku zote, anawalinda watumishi wake wanaomtumikia katika roho na kweli wasipatwe na mabaya.

Mungu akiwa upande wako huna haja ya kuogopa chochote juu ya maisha yako, hata kama vita viinuke juu yako fahamu hivyo vita si vyako bali ni vya Bwana.

Maisha yetu yamefunikwa/kuzungukwa na nguvu ya Mungu.

Samson Ernest.
+255759808081.