“Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari”, Mt 28:19‭-‬20 SUV.

Tuna majukumu mengi katika ufalme wa Mungu, kila mmoja anaweza kusimama kwenye nafasi yake akamtukuza Mungu wake kutokana na kile anafanya mbele zake.

Pamoja na hayo tunapaswa kufahamu kuwa lipo agizo kuu kwa kila mwamini, haijalishi yupoje, ameagizwa kuwafanye wengine kuwa wanafunzi wa Yesu, na kuwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.

Wengi hudhani kazi hii ni ya wachungaji na wainjilisti, tunafikiri hivyo kwa mitazamo yetu tuliyonayo, lakini kwa mujibu wa maandiko hii kazi sio ya watu fulani peke yao, kila mfuasi au mwamini wa Kristo anapaswa kuwajibika kumfanya mwingine kuwa mwanafunzi wa Yesu.

Kanisa linapaswa kwenda ulimwenguni kote na kuhubiri injili kwa watu wote wasiomwamini Kristo kufuatana na agizo la Yesu alilolitoa kwa waamini.

“Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu”, Efe 2:19 SUV.

Kazi hii ya kuwahubiri wengine ni pamoja na kuwatuma wamishenari kwenye kila taifa, ambapo wengine tulijenga mitazamo hasi juu ya hili na kuona ni kazi ya watu fulani tu. Wakati ni wajibu wa kanisa kuwatuma wamishenari au waamini wenyewe kujitoa.

“Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao. Basi watu hao, wakiisha kupelekwa na Roho Mtakatifu wakatelemkia Seleukia, na kutoka huko wakasafiri baharini hata Kipro. Na walipokuwa katika Salami wakalihubiri neno la Mungu katika masinagogi ya Wayahudi, nao walikuwa naye Yohana kuwa mtumishi wao”, Mdo 13:2‭-‬5 SUV.

Kutokana na agizo hili mahubiri mengi yanapaswa kulenga “toba na msamaha wa dhambi” (Lk 24:47), ahadi ya kupokea karama ya “Roho Mtakatifu” (Mdo 2:38) na kuwasihi watu wajitenge na mambo mabaya, wakingojea kurudi kwa Yesu Kristo.

Kusudi la kufanya haya yote ni kuwafanya washirika au wanafunzi ambao watafuata maagizo ya Kristo. Kristo hakusudii kuona matokeo ya uinjilisti na ushuhudiaji wa kimishenari yawe tu ya watu kukata shauri la kuokoka.

Nguvu za kiroho hazipaswi kuelekezwa sana katika kuongeza idadi ya waamini wapya wa kanisa tu, bali kuweka bidii ya kuwafanya watu kuwa wanafunzi wanaoweza kujitenga na dhambi, na kushika amri za Kristo, na kumfuata kwa moyo, akili, na utashi wao.

“Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru”, Yn 8:31‭-‬32 SUV.

Zaidi ya hayo, tunapaswa kukumbuka kuwa Kristo anatuagiza tuzingatie kuwafikia wanaume na wanawake, wazee kwa vijana, waliopotea njia, na sio kuwafanya watu wawe wakristo bila kuelewa kwanini wanamwamini Kristo.

Wale wote wanaomwamini ni lazima waachane na mambo mabaya ya ulimwengu huu wa sasa uliojaa maovu mengi, na kujitenga na upotovu au uovu wa kila aina.

“Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia, basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru. Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake”, Rum 13:12‭-‬14 SUV.

Wale wote wanaomwamini Kristo na injili yake watabatizwa kwa maji, hii inawakilisha agano lao la kuukana uovu, katika ulimwengu huu katika hali yao ya dhambi, na kujitoa kwao kikamilifu kwa Kristo.

Kristo atakuwa pamoja na wale wafuasi wake waaminifu katika uwepo wake na nguvu za Roho Mtakatifu (Mt 28:20) sisi tulioamini tutatakiwa kwenda kushuhudia habari za Yesu kwenye mataifa yote baada tu ya kuvikwa uwezo utokao juu.

“Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi”, Mdo 1:8 SUV.

Hili ndilo agizo la Yesu kwetu waamini au wafuasi wake, tunapaswa kuwagawia wengine kile tumepata neema ya kukipata bure, tunapaswa kufanya juhudi katika kuwafanya wengine kuwa wanafunzi wa Yesu Kristo.

Mahali popote unapofanya kazi, unayo nafasi ya kumfanya mtu kuwa mwanafunzi wa Yesu, ukiwa na malengo na nia utaweza, wengine wanaweza kujiuliza nitawezaje, utaweza, kuhubiri injili sio lazima usiamame kwenye majukwaa makubwa.

Mtaani kwako au ofisini kwako unaweza kumwonyesha uliyenaye naye karibu upendo wa Kristo, vile unamtendea, vile anakuona unaenenda katika mwenendo safi, vile anaona unavuka majaribu mbalimbali, atavutiwa na wewe na kutamani kumjua Mungu unayemwabudu.

Mungu atusaidie sana tuweze kutambua wajibu wetu.
Samson Ernest
+255759808081