Mungu ametupa nafasi ya kumiliki vile vitu amevitengeneza/kuviumba mwenyewe, kupewa nafasi hiyo ya umiliki sio kana kwamba itaondoa nafasi ya Mungu katika hivyo vitu.
Mungu ametupa nafasi na uwezo wa kuwawekea mikono wagonjwa wakapona, Mungu kutupa mamlaka hiyo ya kuombea wenye shida wakapokea uponyaji. Haiwezi kuondoa nafasi ya Mungu katika hayo yaliyotendeka, wala hatuwezi kujichukulia utukufu wowote juu ya hayo matendo makuu.
Haijalishi tutafanya mambo makubwa ya kushangaza ulimwengu mzima, nafasi ya Mungu haiwezi kuondolewa katika hayo. Wala hatuwezi kujivunia hayo mambo makubwa na kuona Mungu hahusiki na lolote.
Kujaribu kuondoa nafasi ya Mungu, na kujaribu kujichukulia utukufu wa Mungu, ni kujitafutia hukumu ya Mungu. Ni kutafuta kuadhibiwa na Mungu, na wote tunajua Mungu akiachilia adhabu yake kwa mtu ni hatari sana.
Haya tunajifunza kupitia Misri na mfalme wake Farao, alifika mahali akasema mto ni wake, wakati Mungu alikuwa ameufanya. Hakuona hilo, yeye aliona ni mto wake na Mungu hakuhusika kabisa na hilo.
Rejea: Nayo nchi ya Misri itakuwa ukiwa na jangwa; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA; kwa sababu amesema, Mto huu ni wangu, nami nimeufanya. EZE. 29:9 SUV.
Ili Misri itambue nafasi ya Mungu, Mungu alidhamiria kuifanya Misri kuwa Ukiwa na jangwa. Hii yote ni kwa sababu ya kuondoa nafasi ya Mungu, na kuona mto ni wao.
Haya yanaweza kumpata mtu yeyote yule, kama atafika mahali akajaa kiburi cha mafanikio na kuanza kuona nafasi ya Mungu haipo kwenye mafanikio yake. Kufika mahali kuona hatua aliyofikia ni kwa sababu ya ujanja wake na akili zake.
Ukishajiona umeanza kutoa nafasi ya Mungu na kutaka uonekane wewe, uwe unajua unaelekea kwenye anguko baya sana. Nafasi ya Mungu haiwezi kuondolewa kwa namna yeyote ile kwa mambo aliyoyaumba yeye mwenyewe, uwezo alioweka ndani ya mwanadamu ni kwa ajili ya utukufu wake.
Lolote utakalopata pongezi, mrudishie Mungu sifa na utukufu wake, usikubali kujiinua wewe, alafu jina la Yesu Kristo likafunikwa na kujiinua kwako. Kufanya hivyo ni kumkasirisha Mungu wako.
Mungu atusaidie sana.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081