Kinywa kina nguvu, kinaweza kunena jambo na likawa, liwe jema au liwe baya. Kile unakiri mara kwa mara, ndivyo utakavyokuwa.
Ukiri wa jambo unatokana na mazingira ya mtu alipo, sio kana kwamba mtu anakuwa mwongo vile ananena. Mara nyingi huwa tunanena maneno kutokana na hali tunazopitia, inaweza ikawa hali nzuri au mbaya.
Tunaposema hali ngumu, ni mazingira yanaonyesha hivyo, sio kwamba tunadanganya, huenda ulipo una hali ngumu kweli. Pamoja na unaona hali ngumu, yupo mtu haoni huo ugumu, hata kama mpo pamoja.
Wakati mwingine sio kana kwamba yule anayeona hali nzuri, ni kwa sababu yeye yupo kwenye hali nzuri. Vile anachukulia mambo, vile anaona ushindi ulio mbele yake.
Mtu huyu anakuwa hasumbuliwi kabisa na kipindi kigumu anachopitia kwa muda huo, maana yeye anatazama lengo lake la kufikia ule uzuri anaouona kwenye maono yake.
Kwa hiyo hali yake ya sasa haimtishi sana, anahakikisha anaendelea kujiweka vizuri na Mungu wake, ili afikie yale malengo yake.
Mtu wa namna hiyo huwezi kumkuta anakiri udhaifu, huwezi kumkuta anakiri kushindwa, na huwezi kumkuta anaungana na marafiki zake waliokata tamaa na yeye awe miongoni mwao.
Ukimkuta yupo miongoni mwa kundi lililokata tamaa, ana kazi maalum kwenye hilo kundi, hata matendo yake ukiyatazama utaona yanaonyesha wazi kuwa ni mtu mwenye ukiri wa ushindi.
Umefika mahali umechoka, huna msukumo wowote wa kuendelea na kile Mungu alikupa ndani yako. Kuanzia sasa kiri ushindi, hata kama unaonekana kwa nje u dhaifu, elewa kwa Mungu haipo hivyo.
Picha gani unaiona kwenye kesho yako, ona una nguvu, ona u hodari, ona ushujaa. Kujiona hivyo utaanza kuona mabadiliko yakitokea ndani yako, utaanza kuona kushinda na sio kushindwa.
Mungu wetu ni mwaminifu, yupo pamoja nasi, hata katika hali duni, tukimwita, yeye atatushindia kwa yote.
Rejea: Yafueni majembe yenu yawe panga, na miundu yenu iwe mikuki; aliye dhaifu na aseme, Mimi ni hodari. YOE. 3:10 SUV.
Sijui umekuwa dhaifu eneo gani, Neno la Mungu linasema useme, mimi ni hodari, na kweli wewe ni hodari.
Ilimradi wewe ni mwana wa Mungu, uliye mwaminifu kwake, uliyeamua kuacha dhambi na kumrudia yeye, na kumfanya kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako. Fahamu wewe ni hodari, na fahamu hivyo kuanzia sasa na siku zako zote.
MUHIMU: Una nia ya kweli ya kusoma Neno la Mungu, na unahitaji ndugu/marafiki wa kuwa nao pamoja katika kusoma Neno la Mungu na kushiriki tafakari yako na wenzako na wao wanatoa zao. Jibu lako lipo Chapeo Ya Wokovu WhatsApp group, wasialana nasi kwa WhatsApp +255759808081.
Mungu akubariki sana.
Imeandikwa na Samson Ernest.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.