Usije ukafikiri watu wanaotenda maovu mbele za Mungu wana amani sana kwenye mioyo yao, hakuna amani yeyote wanayopata ndani yao.

Usifikiri watu wanaofanya mabaya, labda wana amani sana mioyoni mwao, wala usije ukafikiri wanaishi maisha ya furaha sana.

Maisha ya mtenda mabaya, ni maisha yaliyojaa mashaka mengi sana, tena mioyo yao inaweweseka na ubaya waliotenda.

Utulivu kama utulivu haupo kabisa kwa mtenda mabaya yeyote yule, angalia vizuri hili, mfanyie mwenzako baya uone kama utapata utulivu ndani yako, utaona huna utulivu kabisa ndani yako.

Usifikiri mtu anayekutendea baya, yeye anabaki na furaha ndani yake, alafu wewe unaumia. Hakuna kitu kama hicho, hana amani yeyote ndani ya moyo wake, mahangaiko aliyonayo ni makubwa kupita hata wewe.

Kama unafikiri kumtendea mwingine baya, kwa jambo baya alilokutendea, ukafikiri labda utakuwa na amani moyoni mwako kwa kumlipiza kisasi. Utakuwa unajidanganya vibaya sana, huwezi kutenda ubaya ukawa na amani moyoni mwako.

Kutenda ubaya unajiongezea mzigo mbaya ndani yako, mzigo ambao utakukosesha amani siku zote za maisha yako.

Usitende ubaya ukafikiri utakuwa salama, wala usitende ubaya kwa mwenzako ukifikiri unamkomoa. Kwanza unatenda dhambi kwa Mungu, na pili hiyo dhambi itakukosesha amani siku zote, mpaka pale utakapomrudia Mungu wako.

Haya tunajifunza ndani ya Neno la Mungu, sikuelezi habari za kupika, nakueleza maneno ambayo Mungu mwenyewe amesema kupitia Neno lake.

Rejea: Hapana amani kwa wabaya; asema Mungu wangu. ISA. 57:21 SUV.

Usije ukafikiri walevi, wazinzi, washareti, waongo, wachonganishi, wala rushwa, wezi na wengine wengi wenye tabia mbaya zisizo mpendeza Mungu, ukafikiri wana amani sana mioyoni mwao.

Huwezi kuwa na amani kwa kumchukua mume wa mwanamke mwenzio ukamweka ndani, kwa kisingizio cha amejileta mwenyewe hukumwita wewe.

Huwezi kumwacha mke wako ndani, ukaenda kukimbizana na wanawake wengine wa nje, kwa kisingizio chochote kile. Ukafikiri utaipata amani, nakwambia amani hutokaa uipate kamwe.

Huwezi kumdanganya mchumba wako upo vizuri huna mtu mwingine, wakati huo una mtu mwingine unatembea naye kimapenzi kwa siri. Ukafikiri utakuwa na amani kwa hilo unalolifanya, nakwambia kila siku utakuwa unasikia makelele yatakayo kufanya ukose amani kabisa.

Tena wabaya wamefananishwa na bahari iliyochafuka, bahari isiyoweza kutulia, na maji yake hutoa tobe na takataka.

Rejea: Bali wabaya wanafanana na bahari iliyochafuka; maana haiwezi kutulia, na maji yake hutoa tope na takataka. ISA. 57:20 SUV.

Epuka kutenda ubaya wa aina yeyote ile kwa kufikiri utapata amani, hakuna ubaya unaoweza kukuletea amani maishani mwako, japo unaweza kupata mawazo potofu ya kukuvuta utende ubaya/uovu. Lakini fahamu hakuna amani utakayoipata kwa kutenda ubaya/uovu.

Mungu akusaidie kuelewa haya.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081