
Katika vitu ambavyo unapaswa kuwa navyo makini sana ni utoaji wa taarifa ngumu/mbaya.
Kwanini nasema hivi; zipo taarifa kama vile kifo, mtu kuondokewa na mpendwa wake, au mtu wake wa karibu.
Anaweza akawa mzazi, mume, mke, mtoto, mtu aliyeondokewa na mmoja kati ya watu hao.
Mtu huyo hapaswi kupelekewa taarifa kienyeji, bila kuwa na tahadhari kubwa ya namna ya kumweleza kilichotokea.
Usipokuwa makini unaweza kumpoteza kwa mshtuko na yeye unayempa taarifa ngumu.
Kama tunavyoona kwa Eli, kuletewa taarifa ya kilichotokea. Alianguka akavunjika shingo yake na kupoteza maisha yake.
Rejea: Yeye aliyeleta habari akajibu, akasema, Israeli wamekimbia mbele ya Wafilisti, tena watu wengi sana wameuawa, hata na wana wako wawili, Hofni na Finehasi, wamekufa pia, na sanduku la Mungu limetwaliwa. Ikawa alipolitaja sanduku la Mungu, Eli akaanguka kitini pake kwa nyuma, kando ya mlango, shingo yake ikavunjika, akafa; maana alikuwa mzee, tena mzito. Naye alikuwa amewaamua Israeli miaka arobaini. 1 SAM. 4:17-18 SUV.
Utoaji wa taarifa mbaya unapaswa kuwa nao makini sana, hili sio la kupuuza hata kidogo.
Tumemwona Eli akipoteza maisha baada ya kupokea taarifa ngumu.
Tunamwona mwanamke ambaye alikuwa mjamzito, baada ya kupokea taarifa ngumu alipata uchungu wa ghafla na kazaa palepale.
Rejea: Tena mkwewe, mkewe huyo Finehasi, alikuwa mja-mzito, karibu na kuzaa; basi, aliposikia habari ya kutwaliwa sanduku la Mungu, na ya kwamba mkwewe na mumewe wamekufa, akajiinamisha, akazaa; maana utungu wake ulimfikilia. 1 SAM. 4:19 SUV.
Sijui kama unanielewa ninachokueleza hapa, na sijui kama unaelewa hii mistari. Roho Mtakatifu akusaidie uelewe hili jambo ili likusaidie katika maisha yako.
Utoaji wa taarifa kwa mtu au watu, unapaswa kuwa nao makini sana. Ukilipuuza hili linaweza kukuletea au kuzalisha madhara makubwa zaidi.
Hili liwe somo kwetu, utoaji wetu wa taarifa tuwe nao makini sana sana. Itasaidia kuepusha mambo mabaya kwa tunaowapa taarifa.
Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
www.chapeotz.com
+255 759 80 80 81.