2 FAL. 4:2 SUV.

Elisha akamwambia, nikufanyie nini? Niambie una kitu gani nyumbani? Akasema, mimi mjakazi wako sina kitu, ila chupa ya mafuta.

Kila mmoja ana kitu cha kuanzia ili aende hatua nyingine. Hicho hicho uonacho si kitu, ndicho Bwana anataka kuanza nacho.

Huyu mke wa mtumishi alikuwa anapita kwenye changamoto nyingi; ujane, umaskini, upweke na madeni.

Biblia haituambii changamoto hizi alikuwa amedumu nazo kwa muda gani, hasa hii ya kudaiwa deni lililohatarisha watoto wake kuingia utumwani.

Tunachojua ni kwamba kuna siku aliamka akijua pa kuanzia; kwenda kumlilia mtumishi wa Bwana Elisha.

Mchungaji wetu huwa anatufundisha kuwa, tusipite kwenye changamoto wenyewe bali tumshirikishe kuhani wa Bwana/madhabahu ya Bwana.

Kile ambacho mama yule aliona si kitu ndicho Mungu alikitumia kutatua changamoto ya umaskini wake ikiwa ni pamoja na kulipa deni.

Ni kama akina Petro, wale samaki wawili na mikate mitano waliona kama si kitu; lakini ndivyo Yesu alivitumia kulisha wanaume elfu tano mbali na wanawake na watoto.

Ile imani ndogo tuliyo nayo ndiyo hiyo Yesu anasema, tukiitumia, inatosha kuhamisha milima.

Ile sadaka ndogo aliyotia mjane kwenye chombo cha sadaka ndiyo iliyoufunua upendo wake mkubwa kwa Yesu.

Kile kitu tuwapacho watu ndicho hicho anachokitumia Mungu kutujaza baraka za kusindiliwa na kusukwasukwa.

Ile zaka kamili tunayotoa, ndiyo hivyo Mungu anatufungulia milango na madirisha ya mbinguni na kumzuia yule mharibu.

Bwana hajatuacha bila kitu, hata Musa alimwuliza ‘una nini mkononi?’

Hata sisi tulioitwa kumtumikia Mungu, hekima ya ulimwengu yaweza kutuona si kitu, lakini ndio ambao tukisimama vyema hutumiwa na Mungu kuupindua huo ulimwengu wao.

Tumruhusu Mungu atutumie na vyote tulivyonavyo jinsi apendavyo, aonavyo na atakavyo.

Sisi ni wa thamani sana machoni pa Mungu, ndiyo maana anaishi ndani yetu.

By Shealtiely Molla.

WhatsApp +255738858888