Bila shaka umewahi kusikia watu wakisema mtoto huyu ni roho yangu, nampenda sana mtoto wangu, yeye ndio furaha yangu, yeye ndio kila kitu kwangu, na majina mengine mengi sana ya kumsifia mtoto wake na kuonyesha ni jinsi gani moyo wake wote upo pale.

Ukitaka kujua moyo wa mzazi yule kuwa moyo wake wote upo pale, mguse yule mtoto, anaweza kupata mshtuko mbaya sana. Mshtuko ule unaweza kumsababishia kuondoa uhai wake asipokuwa makini, maana upendo wake wote ameukabidhi kwa mwanaye.

Wengine kwa baba au mama zao, wapo watu wanawapenda kweli wazazi wao, kama wapo hai wote utakuta ana upendo sana kwa mama au kwa baba. Wachache sana utawakuta wana upendo kwa wazazi wote wawili, wapo wana upendo sana kwa mama, na wapo wana upendo sana kwa baba zao.

Sio vibaya kuwapenda watu, sio vibaya kumpenda mtoto wako uliomzaa, sio vibaya kumpenda mzazi wako aliyekuzaa au aliyekulea na akakusomesha. Unafanya vizuri kabisa kuwapenda wazazi wako au watoto wako, inategemeana na upendo wako umeuweka wapi sana.

Shida inakuja pale upendo ule unapozidi upendo wa Mungu, yaani unampenda sana baba au mama kuliko Mungu aliyekuumba. Kwa Mungu huna upendo wa kiwango kama unavyompenda baba au mama yako, upendo wako kwa Mungu haupo wa kiwango hicho.

Utasema upendo wangu kwa Mungu haupo vipi wakati mimi ni mkristo, au utajiuliza nitajuaje nina upendo kwa Mungu ama sina upendo kwake. Matendo yako yatakupa majibu ya maswali yako, angalia muda unaoutumia kwa mambo ya Mungu, angalia kujitoa kwako kwa mambo ya Mungu, angalia nguvu unayoweka kwa mambo ya Mungu.

Ukichunguza hayo yote utajua kwa Mungu umeweka nguvu ndogo sana, utakuta hata ukimtenda Mungu dhambi huna msukumo wa kutubu na kuacha kama unavyokuwa na msukumo wa kumpendesha mama au baba yako unapomkosea.

Mtu yupo tayari kufanya lolote kwa ajili ya mtoto wake ila hayupo tayari kufanya kila njia kupata muda wa kutulia na Mungu katika maombi, kusoma Neno la Mungu, kuhudhuria mafundisho ya Neno la Mungu, kutoa sadaka kwa ajili ya kazi ya Bwana. Lakini watu kama hawa wanakuwa wa kwanza kulalamika kwanini Mungu hawasaidii katika shida zao.

Watu kama hawa wanaopenda baba au mama zao kuliko Mungu, mbele za Mungu wanakuwa wamekataliwa tayari. Mtu anayempenda mtoto wake kuliko Mungu, tena anathubutu na kusema mtoto wake ndio kila kitu kwake, huyo mzazi anakuwa amekosa kibali mbele za Mungu.

Mungu anasema mtu wa namna hiyo, hanistahili, kwa lugha nyepesi tunaweza kusema hafai mbele za Mungu. Ikiwa mtu huyu hafai mbele za Mungu au hastahili mbele za Mungu, ni kipi atakiomba kwake akakipewa ikiwa hajui kuwa kuna dhambi imesimama mbele yake bila yeye kutambua kuwa ni kizuizi kwake?

Jibu lipo wazi kabisa, fundisho hili lipo kwa ajili yako, lipo kwa ajili yangu, ndio maana leo unasoma hapa, Neno la Mungu linatusaidia kujua tunakosea wapi na tunapatia wapi. Hata kama ulikuwa unaenenda isivyo sawa sawa, siku ya leo unaweza kujirudi kwa upya kwa kwenda mbele za Mungu kwa kutubu.

Hebu tuone Neno la Kristo linasemaje kuhusu hili jambo ninalokueleza hapa, huenda bado unaona kumpenda baba au mama au mtoto wako sana kuliko Mungu. Ukaona ni jambo ambalo halina tatizo kwako, upendo wa baba, mama, mtoto, hupaswi kuchukua nafasi ya Mungu, yaani upendo wa Mungu unapaswa kuwa wa kiwango cha juu zaidi kuliko vitu vingine vyovyote chini ya jua.

Rejea: Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili. MT. 10:37 SUV.

Jiulize Mungu ana nafasi gani katika maisha yako, upo tayari kufa na kupona kusimama na imani yako ya Kristo, au haupo tayari kumkwaza baba au mama yako ambaye hayupo tayari kukuona ukiwa umeokoka. Ambaye hayupo tayari kukuona ukiwa unamtumikia Mungu wako.

Dada upo tayari kukosa ajira mahali ambapo umemkuta mwajiri anakutaka ulale naye kimapenzi ndipo aweze kukupa ajira au upo tayari kuikosa ajira ili kulinda uhusiano wako na Mungu?

Dada upo tayari kufelishwa na mkuu wako wa chuo au wa somo husika kwa sababu umemkataa kimapenzi, au upo tayari kulala naye ili asifanye kitendo kibaya alichokipanga kwako kukifanya? Kipi cha maana sana kwako, kufaulu mitahani kwa kulala na mkuu wako wa chuo au mwalimu wako wa somo au wa chuo, au upo tayari kulinda uhusiano wako na Mungu.

Yusuf alilinda uhusiano wake na Mungu, Yusuf hakutazama cheo cha mke wa potifa, Yusuf alitazama ule uhusiano wake na Mungu. Upendo wa Yusuf kwa Mungu ulikuwa wa kiwango cha juu sana kuliko nafasi aliyokuwa nayo utumwani, majaribu au changamoto alizokutana nazo hazikumwondoa na hazikumtia hofu ya kuendelea kulinda uhusiano wake na Mungu.

Daniel, Abednego, Shedraka, na Meshaki, hawakutishwa na vitisho vya mfalme Nabukadreza aliyewataka kuabudu sanamu, walisimama na msimamo wao ule ule. Walilinda uhusiano wao na Mungu, hata kama mazingira yaliwataka kuabudu sanamu, wao walisimama kumwabudu Mungu wao aliye hai.

Upendo wako kwa Mungu unapaswa kuzidi vitu vingine vyote, kama kwa Mungu upendo wako upo chini. Na upendo wako kwa kazi yako upo juu zaidi, huwezi kutoa muda wako kwa ajili ya Bwana, huwezi kutoa muda wako kwa ajili ya kusoma Neno la Mungu. Utaona jambo la kawaida tu, ufanye, usifanye, kwako itakuwa sawa tu.

Upendo wako kwa Mungu uzidi wa baba yako, mama yako, mtoto wako, mume wako, mke wako, mchumba wako, kazi yako, ndipo utaona ukimpendeza Mungu zaidi. Utaona akikupa kibali zaidi kwa watu wake, maana hayo yote ni yake, maana hivyo vyote ni vyake, kama utavipenda kuliko yeye moja kwa moja utajitafutia matatizo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
WhatsApp: +255759808081