Wakati bado sijajua umhimu wa hili, nilikuwa nalipuuza sana na kuona ni kitu cha kawaida kabisa ila baadaye nilivyojua umhimu wa kumfuatilia yule aliyeokoka mikononi mwangu. Nikawa nahakikisha nafuatilia maendeleo yake,  japo sio kwa kiwango kikubwa sana huwa nafanikiwa kwa hili ila angalau nafanya.

Wakati nafanya hili sikujua kama kuna andiko ndani ya Biblia ambalo linaelezea hili la kuwafuatilia wale ambao wanaokoka, binafsi nilikuwa nafanya kama jambo ambalo niliona matunda yake baada ya kulifanya.

Wengi wetu tunaweza tukawa tunafanya hili jambo kwenye makanisa yetu, hasa makanisa machanga, yaani yale yanayoanza huduma au yale yanayofungua huduma mpya. Huwa wapo makini sana kufuatilia mshirika mpya aliyeokoka siku za karibuni.

Changamoto ipo kwa yale makanisa ambayo yameshakuwa na washirika wengi, mara machache sana utakuta washirika wapya wanafuatiliwa maendeleo yao. Wengi huwa wanaokoka baada ya muda fulani kupita unakuta wengi wamerudi nyuma.

Yupo mtu hajawahi kuingia maisha ya wokovu, siku anaingia huenda aliingizwa na shida alizokuwa nazo, anapopata suluhisho la mahitaji yake. Anaona moja kwa moja aokoke, anapookoka sasa zipo changamoto atakazokutana nazo kwenye kuokoka kwake.

Anapokutana na changamoto mpya za maisha mapya ya wokovu, bila kuwa na uangalizi wa karibu, mtu huyo ni rahisi sana kurudi nyuma. Unaweza kushangaa alikuwa na moyo kweli wa kuhudhuria kanisani, baada ya muda fulani anapotea.

Tukiwa kama watumishi wa Mungu, tusifurahie kuona watu wakiokoka kwa wingi, alafu hao watu wanaookoka hatuna muda wa kufuatilia maendeleo yao. Ni muhimu sana sisi tukiwa watu waliokomaa kiroho, kuhakikisha wale ambao wanaanza wokovu, tuwe na utaratibu mzuri wa kufuatilia.

Mhubiri anaweza akaja kutoka mahali, akahubiri sana, watu wakaokoka sana, sisi tunaobaki hapo, tunapaswa kuhakikisha wale waliokoka wanakuwa washirika hai.

Wengine tunaenda nao vizuri kabisa, ila watakapobatizwa, huwa tunaona tumemaliza kazi, lazima tujue kuwa bado hatupaswi kuwaacha wale waliokoka. Lazima tuwafuatilie kujua maendeleo yao, ikiwezekana sisi wenyewe tuliowahubiri wakaokoka, tuhakikishe wanaendelea kubaki ndani ya wokovu.

Hili tunajifunza ndani ya Neno la Mungu, sio mtazamo tu ambao mtumishi fulani ameona ni mzuri, hapana, hili jambo lipo kimaandiko kabisa. Tangu zamani ulikuwa ni utaratibu uliofanywa na mitume.

Rejea: Baada ya siku kadha wa kadha Paulo akamwambia Barnaba, Haya! Mrejee sasa tukawaangalie hao ndugu katika kila mji tulipolihubiri neno la Bwana, wa hali gani. MDO 15:36 SUV.

Umeona hapo, Paulo anamsihi Barnaba warudi mahali walipohubiri Neno la Mungu, kuwaangalia maendeleo ya wale waliompokea Yesu Kristo. Inamaanisha hili ni jambo la msingi sana kwa watu wote wanaohubiri injili ya Yesu Kristo.

Kama ulikuwa unachukulia hili jambo kawaida, kuanzia sasa anza kulichukulia kwa uzito mkubwa sana, watu wote wanaookoka mikononi mwako. Hakikisha unawafuatilia, unapomfuatilia utamtia moyo pale amekwama mahali.

Kama kuna mtu ulimshawishi aache dhambi na aokoke, hata kama wewe hukumwongoza sala ya toba, akaongozwa na mtu mwingine, huyo mtu ameokoka mikononi mwako. Unapaswa kumfuatilia kuhakikisha anaendelea na wokovu.

Unapaswa kuhakikisha anahudhuria mafundisho ya Neno la Mungu, na unapaswa kumhimiza kusoma Neno la Mungu kila siku. Mweleze faida yake na hasara yake ya kutokufanya hivyo, utakuwa umefanya sehemu yako.

Kama bado hujajiunga na kundi la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, hujachelewa, tuma ujumbe wako wasap namba +255759808081 utapatiwa maelekezo mengine ya kuweza kuendana na kundi letu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com