Zipo nyakati ngumu ambazo huwa tunapitia hapa duniani, nyakati ambazo zimegubikwa na mambo mengi ya kuumiza mioyo yetu.

Nyakati ambazo zimejaa kudharauliwa na ndugu zetu, rafiki zetu, majirani zetu, jamaa zetu, na wale tunaopata nafasi ya kuwa nao karibu.

Ni nyakati fulani hivi za mateso ndani ya moyo, ni nyakati ambazo zimejaa mafadhaiko makubwa, maana zimesongwa na majaribu yasiyokoma.

Linatoka jaribu moja au changamoto moja na kuingia nyingine, ni kama shida zinapandiana, ni kama shida zinaachiana zamu. Ikitoka shida hii, inakuja shida nyingine.

Jana ulikuwa unalia kwa jambo fulani lililokusibu, kabla hujasahau hilo linakuja jambo lingine la kukuliza tena. Hakuna muda wa utulivu, ukimtazama Mungu unaona kama amekuacha hivi.

Pamoja na hayo yote tunayopitia au tunayoyapata, tunapaswa kuelewa nyakati zote ni za Mungu. Bila kujalisha tunayopitia ni mabaya sana, au yanatuumiza sana.

Daudi baada ya kupakwa mafuta na Samwel ya kuwa mfalme wa Israel. Na baada ya kumuua Goliathi, ni kama alifungulia matatizo yaje juu ya maisha yake yote.

Aliandamwa na mfalme Sauli isivyo kawaida, maisha yake yakawa ya kukimbilia huku na kule kuokoa roho yake. Akawa adui mkubwa wa Sauli, baada ya Sauli kukugundua kitu kwa Daudi, na kitu chenyewe ni ufalme.

Baada ya tabu zote hizo, ilifika wakati Mungu akampa kustarehe, kule kuudhiwa na adui zake. Mungu alizuia hilo lisiwepo kwake kwa wakati huo, ukawa ni wakati wa kustarehe tu.

Wakati yupo kwenye kustarehe kwake, alikuwa anawaza juu ya Bwana, hapa anaonyesha hakujisahau na kuanza kuwa mambo yake mwenyewe.

Akaona kitu cha muhimu sana, akaona yeye anakaa kwenye jumba nzuri la kifalme ila sanduku la Mungu linakaa kwenye mapazia(hema). Kwa maana nyingine haikuwa hadhi yake sanduku la Mungu likae hapo.

Rejea: Ikawa, mfalme alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo BWANA alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote, mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia. 2 SAM. 7:1‭-‬2 SUV.

Watu wengi wanapojikuta wapo kwenye kipindi cha Daudi cha kustarehe, hakuna magonjwa yanayowaandama, hakuna taarifa mbaya za misiba, hakuna hasara kwenye biashara zao.

Kama ni kazini hakuna makwazo mabaya ya kuwafanya waone kazi chungu, hakuna changamoto ya kukosa ada za watoto wao. Mambo yanaenda vizuri kwa ujumla wake.

Kipindi kama hichi sio wote huwa wanaweza kuelekeza mawazo yao kwa Mungu, kutoa muda wao mwingi kusoma neno la Mungu, na kutoa muda wao mwingi kuhudhuria mafundisho ya neno la Mungu.

Sio wote huwa wanakumbuka kumshukuru Mungu, kuona mahali wanaposali wanapaswa kupatengeneza pakakaa vizuri kama zilivyo nyumba zao nzuri. Wanaona uchungu/hasara kutoa kwa ajili ya kazi Mungu.

Daudi alikuwa tofauti kabisa, baada ya Mungu kumpa kustarehe, alianza kuona mambo ya msingi ya kufanya. Ambapo leo tunapaswa kujifunza jambo hili jema, tutaona Mungu akiendelea kutufanikisha zaidi katika maisha yetu na vizazi vyetu.

Mungu akupe kustarehe baada ya tabu.
Samson Ernest
www.chapeotz.com
+255 759 80 80 81