“Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika; Haya ndiyo anenayo yeye azishikaye hizo nyota saba katika mkono wake wa kuume, yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu. Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo; tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka”, Ufu 2:1-3 SUV.
Yesu anajifunua na kuyatathimini makanisa mahsusi saba yasipotee na yasiwavumilie walimu wa uongo, manabii na mitume waliokuwa wanapotosha Neno lake. Barua hizi hazikuandikwa kwa makanisa haya saba kwa sababu yalikuwa jumuiya pekee za Kikristo katika Dola ya Rumi.
Wala hazikuandikwa kwa makanisa hayo pekee, bali makanisa saba yalichaguliwa kwa sababu saba ilikuwa ni namba ya ukamilifu, kwa mtazamo huu tunaweza kusema makanisa haya saba yanawakilisha jumuiya yote ya wanaomwamini Mungu.
Makanisa haya mengi yalikuwa katika mateso mazito, na mengine yalikuwa yanajaribiwa kutafuta mwafaka na taratibu na nguvu za uovu.
Makanisa ulimwenguni kote yanakutana na mazingira kama haya. Mengine yanateswa, waumini wake wakiongezwa katika orodha ya mashahidi wa Kikristo.
Makanisa mengine yanaishi katika mazingira ya ukandamizaji wa kijamii na yanajihusisha katika mapambano magumu ya kubadili hali hizo zinazowakumbuka katika jumuiya zao.
Makanisa mengine kama kanisa la Laodikia yalikuwa matajiri, yenye usalama na kuheshimika, lakini yalikuwa yamefilisika kiroho. Yalibaki na sifa za utajiri wao ila mambo ya kiroho yalishawatoka, jambo ambalo lilikuwa hatari mno kwao.
Tunahitaji kutumia masikio yetu ya ndani kusikiliza Roho anavyoyaambia makanisa, matajiri kwa maskini, walio dhaifu na wenye nguvu, wenye Amani na wanaoteseka na mambo mbalimbali katika maisha yao.
Makanisa saba yalikuwa Zaidi ya mifano tu, pia yalikuwa ni makanisa halisi yaliyokuwepo katika mzunguko wa asili wa msafara wa kale, kuanzia Efeso na kuishia Laodikia. Na kila barua inaweka wazi hali halisi ya mazingira ya kanisa husika lililoandikwa.
Barua hizi zote za makanisa zimeundwa katika muundo mmoja. Kila barua ina sifa yake isipokuwa barua ya Laodikia, imeandikwa kutokana na hali ya kanisa hili ilivyokuwa.
Kukiri ni kitu tunachoona ni kigumu katika huduma zetu na katika maisha yetu ya kila siku. Inaonekana ni rahisi sana kutafuta kosa la mtu kuliko kusifu kwa yale mazuri aliyoyatenda. Lakini barua hizi zinatoa mfano mzuri sana wa kukiri mazuri na kusahihisha makosa yaliyofanyika.
Usawa au uwiano huu wa kusema mazuri na mabaya sio tu wa kibiblia peke yake, unapaswa kutumika hata kwenye huduma zetu za kiroho na maisha yetu ya kimwili, mtu anapotenda kosa kama kuna mazuri aliwahi kufanya yasiachwe kusemwa kwa sababu ya makosa yake.
Udhaifu wa mtu na kuanguka kwake kunaweza kuwa funzo baada ya kugundua mwenendo alionao sasa sio ule wa mwanzo, anapojirudi inaweza ikawa nafasi kwake ya kutofanya kosa hilo tena. Kupitia hayo wengine hukua kiroho na kuongezeka hatua nyingine.
“Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu”, 2 Kor 12:9 SUV.
Lengo haswa za barua hizi lilikuwa kuwatia moyo wapokeaji wa makanisa haya saba wawe na uvumilivu hadi mwisho, wabaki watiifu na waaminifu kwa Kristo. Jambo ambalo ni muhimu sana kwetu leo, pamoja na changamoto zote ndani ya wokovu tunapaswa kuwa wavumilivu na kumtumaini Kristo siku zote.
Barua hizi zote mwisho zimemaliza maneno yake ya mwisho kwa kufanana ambayo ni “aliye na sikio, na asikie neno ambalo Roho ayaambia makanisa”, kigezo kimojawapo cha mtu kutosikia maneno au ujumbe muhimu ni kukosa masikio ila mwenye masikio hana kisingizio chochote.
Kila mmoja hawezi kuwa na kisingizio kwa hili, yule ambaye hana uwezo wa kusikia sauti ya kinywa anayo nafasi ya kutafasiriwa kwa njia ya alama, na wengine kwa njia ya maandishi, kila mtu anapaswa kusikia na kuenenda vile Mungu anataka.
Mtu anayepuuza maagizo ya Mungu hapaswi kuwa na kisingizio cha kutosikia, maana hakipo tena, kila mmoja anapaswa kutii na kuishi maisha yanayompendeza Mungu, na yule aliyegeukia maisha ya dhambi anapaswa kujirudi.
Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia yako
Mungu akubariki sana
Samson Ernest