Leo napenda tukumbushane mambo ya msingi sana, habari za kifo zinaweza zisiwe njema sana kwako. Lakini hatutaacha kuzizungumzia maana kifo kipo mbele yetu, itafika wakati ambao utaondoka hapa duniani.

Kuna wakati huwa tunajisahaulisha kuhusu kifo, sio jambo la kufikiria kila wakati hadi ukose raha, hata utakapokumbuka kuwa kuna kifo, hupaswi kukosa raha. Unachopaswa kufanya ni kujiweka vizuri na Mungu.

Kwa kuwa kufa kupo, tunapaswa kujiandaa, kuweka mambo yetu vizuri, kuhakikisha mambo yako ya kawaida kabisa kama vile mali zako, watoto wako, mke wako, unawaweka vizuri.

Kufanya hivyo hakumaanishi kuwa wewe utatangulia na wao watabaki, unaweza kufanya maandalizi hayo ukaendelea kubaki na wao wakawa wametangulia.

Hayo ni maandalizi ambayo anapaswa kuwa nayo mtu kila siku, maana vipo vifo vinatujia ghafla bila kujiandaa kwa chochote.

Maandalizi mengine ni pale unapopewa taarifa na Mungu, wapo watu ambao huwa wanapata neema ya kuandaliwa juu ya kuondoka kwao duniani, wanaelezwa na cha kufanya kabisa kabla hawajafa.

Hili tunajifunza kutoka kwa mtumishi wa Mungu Hezekia, Hezekia alipata neema ya kupata taarifa ya kifo chake. Sio kupata tu taarifa, alipewa jukumu la kufanya kabla ya kufa.

Rejea: Siku hizo Hezekia akaugua, akawa katika hatari ya kufa. Isaya, nabii, mwana wa Amozi, akamjia akamwambia, BWANA asema hivi, Tengeza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. 2 FAL. 20:1 SUV.

Unaona hilo andiko, linatuonyesha wazi kuwa Mungu anaweza kumpa mtumishi wake taarifa za kifo chake. Sio tu taarifa, tunaona lengo la taarifa hii ilikuwa Hezekia kufanya maandalizi ya nyumba yake.

Sijui kama unanielewa hapa kuhusu maandalizi, unaweza usielewe sana leo ila Roho Mtakatifu akusaidie uweze kuelewa hichi ninachokueleza hapa.

Hasa wewe ambaye hujui kama utapata neema kama ya Hezekiah, unapaswa kujiandaa, maana yake kila siku kwako iwe ya maandalizi ya safari. Hii itakufanya kuweka mambo yako vizuri na kuyaishi maisha matakatifu yenye ushuhuda mwema.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
www.chapeotz.com
+255759808081