Jambo lolote ukitaka lidhihirike kuwa ni la uongo au ni la ukweli, usiwe na haraka sana, lipe muda, muda ndio utakaoamua hilo jambo ni la ukweli au ni la uongo.

Uongo utabaki kuwa uongo, na ukweli utabaki kuwa ukweli, haijalishi huo ukweli utachukua muda mrefu kudhihirika wazi. Amini ukweli na uongo utadhihirika tu, hata kama uongo utaonekana kudumu sana, uwe mvumilivu.

Hawa manabii wanaotabiria watu Mungu amesema Mwaka huu hutopita lazima uolewe, mwaka unaisha humwoni huyo mwanaume. Mungu anasema, mwaka huu lazima upate kazi nzuri, mwaka wa tatu sasa hujaiona hiyo kazi. Ujue umekutana na nabii feki.

Nabii wa kweli hana mbwembwe, tena ana hofu kweli kutamkatamka ovyo, tena nabii wa kweli hatumii nguvu nyingi sana. Tena hana mabishano mengi, anasema tu kwa kiasi na mengine anamwachia nafasi Mungu.

Hili tunalithibitisha kwa nabii Yeremia baada ya kutokea nabii Hanania kunena kinyume, nabii Yeremia hakutaka kushindana naye sana na nabii Hanania, alichomwambia asubiri unabii upi utatimia.

Rejea: Nabii atabiriye habari za amani, neno la nabii yule litakapotokea, ndipo nabii yule atakapojulikana, kuwa BWANA amemtuma kweli kweli. YER. 28:9 SUV.

Nabii Yeremia hakuwa na wasi wasi juu ya unabii wake alioutoa, maana alijua unatoka kwa Mungu, ndio maana hakuanza kushindana na nabii mwenzake Hanania.

Kwa kiswahili cha leo, hakutupiana maneno ya majigambo kumwonyesha yeye ndiye nabii wa Mungu. Alichofanya nabii Yeremia, ni kumwambia ule unabii utakaotimia ndio utakuwa unabii wa kweli.

Baada ya siku kupita, ikaja kuonekana nabii Yeremia alitabiri ukweli, na nabii Hanania alitabiri uongo. Yaani Mungu hakumtuma ila alijituma yeye kusema Mungu amesema.

Rejea: Kisha nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, Sikia sasa, Ee Hanania; BWANA hakukutuma; lakini unawatumainisha watu hawa maneno ya uongo. YER. 28:15 SUV.

Leo tuna akina nabii Hanania wangapi Tanzania wanaosema Mungu anasema hivi, mwaka huu utajenga nyumba nzuri, Mungu amesema mwaka huu lazima uende ulaya. Lakini yote uliyoambiwa hakuna lililotimia hata moja.

Mungu gani anayesema uongo? Huyu Mungu ninayemwabudu mimi huwa hasemi uongo, Mungu wa nabii Yeremia hakusema uongo. Ila mungu wa nabii Hanania alisema uongo.

Ulitabiriwa Mungu amesema mwaka huu lazima mume wako arudi nyumbani, ila mwaka umeisha mpaka sasa mume wako hajarudi. Huo ni unabii wa Hanania sio unabii wa Yeremia, nabii Yeremia alikuwa anasema kweli.

Lazima ufike mahali ukue kiakili na kiroho, haina haja kuambiwa na mtu mahali ulipo sio mahali sahihi, umetabiriwa mambo mengi sana na huyo nabii wako. Hakuna linalotimia muda ukifika, uliambiwa mwaka hutoisha utakuwa umepata mtoto ila hakuna kilichokea hadi sasa.

Mungu anaendelea kutufundisha namna manabii walivyo, kuna makundi mawili ametufundisha katika kitabu hichi cha Yeremia, la kwanza ni manabii wa ukweli na la pili ni manabii wa uongo.

Ushindwe mwenyewe kung’amua ila Mungu tayari amelifunua NENO lake kwako. Kama ni chakula, amekuwekea kila kitu mezani, kazi yako ni kula au kutokula.

Mungu atusaidie.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081