
Zipo njia ambazo ukipitia ile hamu ya kufanya kile kilichokupeleka ukakifanye, inaweza ikatoweka kabisa.
Wapo watu ukikutana nao kwenye safari yako ya wokovu, unaweza kugairi kuendelea kumtumikia Mungu wako, au unaweza ukahairisha kuendelea kuishi maisha yanayompendeza Mungu.
Wapo marafiki ambao ukikutana nao, hutakuwa na ule moto wa kuendelea kumtumikia Mungu wako. Wanakuwa wamekunyonya nguvu zako kwa maneno yao kukuvunja moyo, kwa kufikiri walichokueleza ni cha kweli.
Zipo changamoto ngumu Mungu akiziruhusu kwenye maisha ya mtu, mtu huyo hatakuwa na uwezo wa kulitaja jina la Yesu kwa ujasiri. Maana atakuwa ameanguka kwenye dhambi ambayo itaendelea kumkandamiza, kila akitaka kurudi kwenye hali yake ya mwanzo anashindwa.
Habari njema ni kwamba haya yote Mungu huyaona kwa watoto wake wanaomcha katika roho na kweli. Anajua kabisa akiruhusu jambo fulani limpate mtoto wake ndio utakuwa mwisho wake wa kuendelea kumtumikia yeye.
Hili tunajifunza kupitia maandiko matakatifu, kuna mahali Mungu aliwazuia wana wa Israel wasipite kwenye njia ambayo ingewaletea shida.
Rejea: Ilikuwa hapo Farao alipokwisha kuwaacha watu hao waende zao, Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije wakaghairi watu hawa hapo watakapokutana na vita, na kurudi Misri; lakini Mungu akawazungusha hao watu kwa njia ya bara kando ya Bahari ya Shamu; wana wa Israeli wakakwea kutoka nchi ya Misri hali wamevaa silaha. KUT. 13:17-18 SUV.
Nataka ujifunze hapo, nimependa hili andiko; Mungu hakuwaongoza kwa njia ya nchi ya Wafilisti, ijapokuwa ilikuwa ni ya karibu; maana Mungu alisema, Wasije wakaghairi watu hawa hapo watakapokutana na vita, na kurudi Misri
Ilikuwepo njia ya karibu sana kupita wana wa Israel ila Mungu hakutaka wapitie huko wasije wakakutana na vita wakarudi tena Misri.
Hii inatufundisha nini katika maisha yetu ya wokovu? Ni kwamba Mungu anajua kabisa kuna jambo ukilifanya lazima utarudi kwenye maisha yako ya uasherati, uzinzi, ulevi, uongo, useng’enyeji, na mengine mengi mabaya yanayofanana na hayo.
Mungu wetu anatupenda sana, hataki turudi Misri, yaani yale maisha ya kutompendeza yeye, yale maisha ya kukosa uhuru wa kumwabudu yeye, yale maisha ya mateso makali katika utumwa.
Nakusihi sana uendelee kushikamana na Yesu Kristo, yapo mambo mengi sana mabaya hayatayaruhusu yakutokee wewe. Bali atakuongoza kila hatua ya maisha yako ya wokovu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com