Kuna siku moja ndugu mmoja akaniandikia sms, hiyo sms nilivyoisoma ilikuwa inaonyesha mtu aliyevunjika moyo kweli kweli.
Akaniambia mtumishi naomba uniombee nipate mume, naona maombi yangu ninayoomba ni batili mbele za Mungu. Maana kila mwanaume anayekuja kwangu kwa nia ya kunioa, ananikimbia.
Baada ya kusoma ule ujumbe wake, moja kwa moja Roho Mtakatifu alinipa ufahamu juu ya tatizo lake. Nikamuuliza, je! Hao wanaume wote waliokuja kwako, mlikuwa mnafanya nao uasherati kwanza au walikuwa wanakukimbia tu?
Jibu alilonipa ndio lile ambalo tayari nilishapata ufahamu juu ya shida yake ipo wapi, kweli akaniambia kuwa huwa wanafanya nao uasherati.
Fikiri huyu ndugu, anafikiri Mungu hamsikii maombi yake, wakati huo kila mwanaume anayekuja kwake lazima wafanye naye mapenzi.
Na wote wanaokuja kwake kwa gia ya kumwoa, wakimaliza shida zao, wanamwacha hapo. Bila kujua shida yake ipo wapi, yeye anaona Mungu hamjibu maombi yake.
Baada ya kunijibu anachofanyaga, nilimweleza moja kwa moja ukweli, nikamwambia, “hilo ndio kosa lako unalofanyaga” huwezi kumwomba Mungu akakupa haja ya moyo wako. Huku unachanganya mambo.
Kama nisingepata ufahamu wa shida yake, ningemfariji tu kwa maneno mazuri, na kumwahidi nitamwombea kama alivyotoa ombi lake, huku anaendelea kufanya uchafu wake.
Mungu hawezi kusikia sala za mtu anayeendelea kufanya dhambi, hadi pale atakapoamua kutubu dhambi zake na kuamua kuziacha. Usijidanganye kumwomba Mungu akupe mume/mke mwema, wakati huo uliyenaye au kila anayekuja mbele yako, lazima mfanye naye ngono kwanza.
Tena dhambi zako zina uwezo wa kuzuilia mema yako yasikupate, sio kama nakueleza vitu ambavyo havipo. Unaweza kusema hakuna kitu kama hicho, nakwambia kipo kabisa, shida yako hujaona hili andiko.
Rejea: Maovu yenu yameyageuza haya, na dhambi zenu zimewazuilia mema msiyapate. YER. 5:25 SUV.
Umeona huo mstari, ile B yake inasema hivi; Na dhambi zenu zimewazuilia mema msiyapate.
Dhambi ina uwezo wa kuzuilia mema ya Mungu yasikupate, unaweza kukazana kumwomba Mungu akutendee jambo fulani. Kama haupo tayari kutubu na kuacha maovu yako, uwe na uhakika umejiwekea mpaka mwenyewe na Mungu wako.
Mungu akupe kuona haya.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081