Wapo watu ni wataalum wa kuvumisha habari ambazo hawana uhakika nazo, habari ambazo wamesikia watu wakisema.

Bila kujalisha waliokuwa wanasema wana nia njema au wamepika tu habari ya kumchafua yule mhusika ambaye amezushiwa jambo.

Wapo watu wanakuwa wanajua wanachofanya wanakuwa wanatumia nguvu ya umma kusambaza habari isiyo ya kweli.

Na wazushaji wa habari huwa wanatumia nguvu kubwa kusambaza hiyo habari, nia ni iwafikie wengi zaidi.

Kwa sehemu kubwa habari ya uongo huwa inakuwa inaaminika kwa Wale ambao hawana muda wa kutafakari mambo.

Hasa habari za uzushi huwa zimepikwa haswa, msikiaji anapoisikia lazima masikio yake yamwashe. Yanapowasha anakuwa na hamu ya kumsambazia na mwingine.

Sisi kama wana wa Mungu, tuliozaliwa mara ya pili hatupaswi kufanana kama mataifa, yaani wasiomjua Kristo.

Hatupaswi kuwa sehemu ya kuzusha au kueneza habari za uongo, kueneza habari za uongo unakuwa unamkosea Mungu wako.

Rejea: Usivumishe habari za uongo; usitie mkono wako pamoja na mwovu, kuwa shahidi wa udhalimu. KUT. 23:1 SUV.

Umesikia habari zozote ambazo hujajidhirisha nazo, usiwe sehemu ya kuzisambaza hovyo, kuanza kuzisambaza unakuwa kwenye kundi la kuvumisha/kueneza uongo.

Na kama umekuwa mtu wa kutengeneza habari za uongo kwa nia ya kuwachafua wenzako, uwe na uhakika mashimo unayowachimbia wenzako. Mashimo hayo hayo yatatumika kukufukia mwenyewe.

Rejea: Wameweka wavu ili kuninasa miguu; Nafsi yangu imeinama; Wamechimba shimo mbele yangu; Wametumbukia ndani yake! Zaburi 57:6

Acha kabisa hii tabia kama unayo na epuka sana huu mtego mbaya, jifunze kuutafuta ukweli wa jambo au jenga utaratibu wa kujithiridhisha jambo kwanza.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com