Mtu anapokuwa mkubwa, anaweza akawa mzazi wako, au anaweza akawa kiongozi wako kazini kwako.
Akakueleza kuwa ana uhitaji wa kitu fulani bila kukuambia wewe ndiye unapaswa kumletea, ukiwa kama mtenda kazi wake, ama ukiwa kama mtoto wake. Unapaswa kuchukua hatua ya haraka kumletea kile ambacho ana uhitaji nacho.
Mara nyingi mtu anapokuwa na nafasi fulani, ama anapokuwa na umri fulani, kama mzazi au kiongozi. Huwa hawanyooki moja kwa moja, wakitaka mtu mwenyewe ajitolee kufanya kile anahitaji.
Hata kwa mtumishi wa Mungu Daudi ilikuwa hivyo, hili tunajifunza kutoka kwake kibiblia. Alitamani kunywa maji ya kisima cha Bethlehemu.
Angalia sasa vile alisema huyu mtumishi wa Mungu, vile alizungumza na askari wake. Utajifunza kitu kikubwa sana cha kiMungu cha kukusaidia kuweza kumwelewa mtu wa namna hii.
Rejea: Daudi akatamani, akasema, Laiti mtu angeninywesha maji ya kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango! 2 SAM. 23:15 SUV.
Unaona neno lililotumika hapo, “LAITI MTU” hakutoa maagizo ya moja kwa moja nataka fulani akaniletee maji ya kisima cha Bethlehem.
Ona sasa kupitia mstari huu hapa chini, vile askari wake walimwelewa na kuchukua hatua ya kwenda kuleta kile Daudi alikuwa anakihitaji.
Rejea: Basi hao mashujaa watatu wakapenya jeshi la Wafilisti, wakateka maji kutoka kile kisima cha Bethlehemu, kilicho karibu na lango, wakayachukua, wakamletea Daudi; walakini yeye hakukubali kuyanywa, akayamimina mbele za BWANA. 2 SAM. 23:16 SUV.
Sijui kama kuna kitu unakielewa hapa, kuna darasa la msingi sana hapa, hasa wale ambao wapo karibu na viongozi wao, au wazazi wao. Kauli kama hizi zinapozungumzwa na kiongozi au mzazi, inakuwa rahisi kwao kuelewa.
Mungu akusaidie uweze kuelewa lugha kama hizi za fumbo, utakuwa baraka sana kwa mzazi/kiongozi wako.
Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
www.chapeotz.com
+255 759 80 80 81