Lakini mambo yote na yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu. 1 Kor 14:40 SUV

Zipo taratibu ambazo jamii na kanisa zimejiwekea kwa ajili ya kijana kuingia kwenye ndoa, utaratibu huu sio kwa ajili ya kumkomoa kijana wa kiume au binti. Utaratibu huu ni kwajili ya usalama wake na kuonyesha heshima ya tendo hilo jema.

Hizi taratibu si zote ni nzuri, zingine ni mbaya na zinamkosea Mungu, pia zipo taratibu nzuri na ambazo hazimkosei Mungu. Hizi ambazo hazimkosei Mungu ndizo tutakazozijadili sana hapa.

Kufuata utaratibu sio jambo baya, japo inaweza kuonekana sio jambo la muhimu sana kwa baadhi ya vijana au walezi au wazazi au wana jamii. Lakini mtu anayeelewa mambo jambo hili hawezi kulipuuza hata kidogo, hata ukisoma habari za Isaka na Rebeka utaona vile utaratibu ulifuatwa hadi kuoana, vilevile kwa Yakobo wakati anaoa alifuata utaratibu.

Kama tulivyoanza na andiko letu la utangulizi kila jambo linapaswa kwenda kwa utaratibu, ukivunja utaratibu kuna gharama zake, yupo anaweza kuwa alivunja utaratibu na huoni madhara yake. Lakini ukikaa naye utajua kuna kitu hakipo sawa, asipokuwa karibu na Mungu atakuwa anapata shida, na itambidi afuate baadhi ya hatua.

Upo uzuri kama kijana kufuata utaratibu uliowekwa na kanisa na familia yako au ukoo wako, kama nilivyosema utaratibu huu hujawekwa kumkomoa kijana. Naamini hivyo kwa sababu nimeona faida yake, japo baadhi ya watu wanaweza kuutumia vibaya ila kusudi lake sio hilo.

Tuangalie faida zifuatazo za kufuata utaratibu unapotaka kuoa/kuolewa;

1. Unaheshimika.
Hashima ya mtu inajengwa na mtu mwenyewe, wakati mwingine tunasema heshimu ni kitu cha bure, kwa upande mwingine sio kweli. Heshima ina gharama ambayo mtu anakuwa ameitoa hadi kuwa na hiyo heshima, kama ni kijana basi anakuwa ametunza maisha yake ya ujana ndipo anakuwa na heshima.

Unapofuata hatua za kikanisa na za kifamilia, unajiwekea heshima nzuri sana, huu utakuwa msingi wako kwenye ndoa yako. Msingi ambao utakuwa umeishika ndoa yako vizuri, hata inapotaka kuleta shida utakuwa na watu walio nyuma yako, na utakuwa huna hofu ndani yako.

Ndugu wa mke/mume wako wataanza kukuheshimu tangu siku ya kwanza, watakuona na kukuchukulia kwa namna ya tofauti kabisa. Hii itakuwa heshima kwako, wakati mwingine dharau zinaanza kuwafuata wanandoa wengi kwa sababu ya kudharau haya.

2. Kinga kwako.
Wanasema kinga ni bora zaidi kuliko tiba, unapofuata taratibu inakuwa kinga kwako kwa mwolewaji na mwoaji, kama tunavyojua suala la kuoa/kuolewa sio japo dogo. Ni jambo kubwa na pana linalobeba maisha ya mtu kimwili na kiroho, unaweza kuwa imara zaidi kiuchumi unapokuwa na ndoa imara, na unaweza kuwa imara zaidi kwa mambo ya Mungu au huduma unapokuwa na ndoa imara.

Unapokuwa katika mchakato wa kufuata taratibu zilizowekwa, unaweza kubaini kitu kisicho cha kawaida, unaweza kubaini afya ya mwenzako sio salama. Unapojua hilo unakuwa umeshajua cha kufanya kabla ya kuingia naye kwenye ndoa.

Unaweza kubaini tabia yake sio nzuri wakati mnaendelea na michakato mbalimbali ya kuingia kwenye ndoa, hii inakuja kwa sababu wakati mwingine huwa tunavutiwa na macho zaidi na kujikuta tumependa.

Yapo mambo mengine huwezi kuyabaini usipopitia mchakato, unapopitia hatua mbalimbali zilizowekwa na kanisa, zinakusaidia wewe kijana unayetaka kuoa/kuolewa. Wengine wakisikia kwenda kwa mchungaji wanaona bora wavunje mahusiano hayo, hiyo inakuwa salama kwako.

Jambo lingine inaweza kutokea ukapata shida kwenye mahusiano yako, kwa kuwa ulifuata utaratibu, jambo lako litamalizwa katika mazingira mazuri na hutabeba mzigo peke yako. Watumishi wa Mungu na familia yako wanapoungana pamoja kwa ajili ya shida iliyokupata inakuwa salama kubwa kwako, kuliko yule aliyekuwa anafanya bila utaratibu.

3. Unaweza kubaini chaguo lako.
Katiba mchakato wa kwenda kanisani, na kwenda kwa wazazi wako au walezi wako, hapo njiani unaweza kubaini vitu, si unajua wakati mwingine vijana huwa tunaendeshwa na mihemko. Sasa kwa kuwa umekuwa mwaminifu kwa kufuata utaratibu Mungu anaweza kukusaidia ukagundua uliyenaye sio mtu sahihi wa kuishi naye.

Wengine huwa wanajificha au wanaficha tabia zao, mnapoendelea na michakato mbalimbali utagundua baadhi ya tabia kupitia viongozi wa kanisa, au familia yako, au kupitia jamii inayokuzunguka au inayomzunguka yeye.

Inawezekana ulikuwa na hofu, lakini unapoendelea na hatua mbalimbali za kikanisa na kifamilia ile hofu juu ya mwenzako ikaondoka na kumwona ni mtu sahihi kwako wa kuishi naye au kuingia naye kwenye ndoa.

Faida nyingine katika hili mwenzako anaweza kukataa au kukukimbia, inaweza ikawa habari mbaya kwako ila kwenye maisha yako inakuwa habari njema kwa baadaye. Unaweza usijue sana kwanini yametokea hayo ila utakuja kubaini baadaye halikuwa chaguo lako sahihi, inakuwa salama yako.

Hizo ni faida chache na muhimu unazoweza kuzipata kwa kufuata utaratibu wakati wa kuoa/kuolewa, tusiwe tunazipuuza na kuziona hazina maana. Unaweza kusaidiwa na wazazi wako au mchungaji wako wakati umeenda kwao, ukawa umeokoka na mambo magumu mbele yako.

Usimwone mchungaji ni adui yako, wala usione wazazi/walezi wako ni adui yako, washirikishe katika mchakato wako mzima waupe baraka na kukupa maelekezo kadhaa yanayotakiwa ili ufanikishe jambo lako jema.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
+255759808081