Wakati mwingine mtu anaweza akawa na hamu ya watu wengine kuzisema habari zake njema.

Asipoona watu wakifanya vile anatamani iwe, anaweza akaanza kupata shida moyoni mwake kwa hilo.

Kupata kwake shida kunaweza kusababisha baadhi ya madhara katika maisha yake.

Kama alikuwa anajituma kwenye eneo fulani la huduma au kazi, baada ya kuona watu hawafanyi vile anataka. Utamwona anaacha kabisa kufanya lile alikuwa anafanya.

Ukimuuliza shida gani imemfanya aacha kuwajibika ipasavyo. Atakakwambia watu hawanioni, watu hawanijali, na malalamiko mingine mengi.

Ndugu msomaji wangu, haina haja kuwasukuma watu kwa nguvu wakupe sifa zako njema kwa wengine.

Wao wenyewe bila kusukumwa na mtu yeyote, bila kuambiwa semeni hivi na vile, watatoa sifa zako njema.

Ikiwa una sifa mbaya wataambiana, na ikiwa una sifa njema napo wataambiana.

Hizo sifa zako njema unaweza usijue kama zinasambazwa na ndugu zako wa karibu wanaokufahamu.

Hili tunaliona kwa Ruthu, anaambiwa na Boaz kuwa alishaelezwa sana yale aliyoyafanya.

Rejea: Naye Boazi akajibu, akamwambia, Nimeelezwa sana yote uliyomfanyia mkweo, tangu alipokufa mumeo; na jinsi ulivyowaacha baba yako na mama yako, na nchi yako uliyozaliwa, ukawafikilia watu usiowajua tangu hapo. RUT. 2:11 SUV.

Hili litusaidie katika maisha yetu, maana tunaweza tukawa tunataka kutumia nguvu nyingi sana kutaka watu watuseme vizuri.

Ukweli ni kwamba hata tusipotumia nguvu zetu kujulikana, watu wenyewe watatusema vile tulivyo.

Unaweza ukawa na wasiwasi juu ya zile taarifa zinazopelekwa kwa ndugu zako au marafiki zako, labda zinaweza zisiwe nzuri sana, nakuhakikishia ukweli utabaki kuwa ukweli.

Hata kama yupo atajaribu kukuchafua, yaani kusambaza habari mbaya juu yako. Itafika wakati sifa zako njema zitakuwa wazi.

Na kama watu watajitahidi kukupa sifa ambazo sio zako, itafika mahali ukweli wote utakuwa wazi na watu watatambua kuwa waliyokuwa wanaambiwa sio ya kweli.

Bidii yako katika huduma, kazi, kuwatendea wengine mema, sifa zako njema zitajisambaza zenyewe bila wewe kuomba wazisambaze.

Ishi vile Mungu anataka kupitia neno lake, utaona mafanikio yako ya kiroho na kimwili yakienda juu.

Utafika mahali unahitaji msaada, Mungu atakupa kibali mahali sahihi pa wewe kupata msaada huo. Kama tulivyoona kwa Ruthu.

Rejea: Tena wakati wa chakula huyo Boazi akamwambia, Karibu kwetu, ule katika mkate wetu, na ulichovye tonge lako katika siki yetu. Basi akaketi pamoja na wavunaji, nao wakampitishia bisi, naye akala akashiba, hata akasaza. Naye alipoinuka tena ili aende kuokota masazo, huyo Boazi aliwaagiza vijana wake akisema, Mwacheni aokote hata kati ya miganda, wala msimkemee. RUT. 2:14‭-‬15 SUV.

Haya ni matunda ya mwana wa Mungu aliyemwaminifu, katikati ya uhitaji wake anaweza kupata kibali cha namna hii.

Mungu akubariki sana.
Samson Ernest.
www.chapeotz.com
+255 759 80 80 81.