Mtu akifanya vizuri ni vizuri akapewa hongera zake, au ni vizuri ukamsifia kutokana na jambo jema alilolifanya. Ama kutokana na kazi yake njema, ama kutokana na bidii yake njema.

Vibaya sana kukaa na sifa njema ya mtu bila kumwambia, na wakati una uwezo wa kumweleza vile anajitoa, vile anafanya vizuri.

Sasa wengine huwa tunasubiri mtu afe ndio tunaanza kutoa sifa zake njema, kuna watu wanakufa kwa sababu ya kukosa maneno mazuri kutoka kwa watu wao wa karibu.

Pamoja na kuona kumpa sifa njema, au kumpa hongera kwa kazi nzuri, au kwa bidii yake nzuri. Natamani tufikiri kwa pamoja mimi na wewe hapa.

Kwa sababu kuna watu kumpongeza ni kama vile umemwambia afanye vibaya, ni kama umemwambia awe mtu mbaya.

Watu wa namna hii wapo, kumsifia ni kumharibu kabisa, alikuwa hana kiburi, baada ya kumsifia kiburi kinahamia kwake.

Alikuwa mtu mnyenyekevu na mtiifu ila baada ya kumsifia au kumpa hongera, anaharibika kabisa na kuanza kujiona hakuna kama yeye na anawaona watu wote ni takataka.

Kama nilivyotangulia kusema hapo awali kumpongeza mtu ni vizuri sana akiwa hai, ila hebu fikiri utamwongezea hatua au utamharibu kabisa.

Nakuachia na hiyo fikiri ya leo, iwe msaada hata katika malezi ya watoto wako, maana wapo watoto wanakosa adabu kwa kiburi cha kusifiwa na wazazi wao.

Hii ikusaidie kupanua ufahamu zaidi na ujue mazingira gani unapaswa kumpongeza mtu, na mazingira gani hupaswi kumpongeza mtu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com
+255 759 80 80 81