
Mtu anaweza akawa na malalamiko fulani, malalamiko ambayo yanaonyesha kunyimwa kitu, au kunyimwa nafasi.
Malalamiko ambayo mtu mwingine akimsikiliza, na huyo mtu anayemsikiliza akawa hamjui vizuri. Akamsikiliza bila kusikiliza upande wa pili unaolalamikiwa, mtu huyo anaweza kuona kweli anachosema huyo mtu.
Na yupo anachosema kuhusu jambo fulani labda la kunyimwa nafasi au kitu, anachosema ni kweli kabisa. Tena inawezekana anachokuambia na wewe unasema kweli, maana unaujua ukweli wote wa pande zote mbili.
Sasa leo napenda kukufikirisha jambo hili, hivi umewahi kufikiri hayo unayolalamikia, au hilo unalolamikia, ukipewa nafasi wewe utaweza?
Fikiri tu, labda unalalamika juu ya kutopewa nafasi, hiyo nafasi ukiipewa utaitendea kazi? Ukweli unaujua wewe ndani yako.
Labda unalalamika juu ya kutotambuliwa kwako, je ukitambuliwa unafikiri kipo kitu cha kuonyesha kweli kutambuliwa kwako kulikuwa kwa muhimu?
Wakati mwingine unaweza ukawa unalalamikia hayo. Kumbe Mungu anajua kabisa bado unapaswa kujifunza zaidi ili uweze kufiti kwenye eneo unalolitamani uonekane.
Unachotakiwa kujua kila jambo na wakati wake, sio kila kikwazo unachokutana nacho kwenye maisha yako kinatokana na hila za Shetani. Vipo vikwazo vimeratibiwa na Mungu mwenyewe, ili kukupika au kukutengeneza na kukuandaa kwenye nafasi husika.
Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
Mtenda kazi katika shamba la Bwana.
WhatsApp +255759808081
www.chapeotz.com