Yesu asifiwe, Bwana ni mwema sana ametupa nafasi ya kuiona siku ya leo, tuna kila sababu ya kumshukuru kwa matendo yake makuu kwetu.

Asilimia kubwa kila mmoja wetu ana kitu cha kufanya, hata kama kinaonekana ni cha kawaida kipo anafanya.

Wapo hawajawahi kufikiri wanachofanya leo kina mchango mkubwa sana katika maisha yao ya miaka 3 ijayo, miaka 4 ijayo, miaka 5 ijayo, na kuendelea.

Unachofanya leo kiwe kizuri au kiwe kibaya, uwe unaonekana au uwe huonekani, ama uwe unatambulika au uwe hutambuliki.

Uwe na uhakika miaka kadhaa ijayo kitaonekana kwa uwazi ulichokuwa unakifanya, kile unapanda leo katika maisha yako. Uwe na uhakika utavuna matunda yake.

Hebu fikiri kile unafanya leo kinaweza kukuzalia matunda ambayo upo tayari watoto wako wale? Upo tayari wajukuu zako waje wajivunie matunda ya kazi ya mikono yako?

Hebu fikiri kile unakifanya kwenye ukurasa wako wa facebook, Twitter, instagram, LinkedIn, nk upo tayari watoto wako kuja kukitazama na kujifunza jambo?

Fikiri tu, upo nyumbani kama mfanyakazi kazi wa ndani, hilo halina shida, ufanyaji wako wa kazi kuna kitu unakujengea?

Baada ya miaka 5 ijayo kuna kitu cha kujivunia kilichotokana na utendaji wako wa kazi za ndani? Ama unaona kazi unayofanya si ya maana sana.

Chochote unachofanya leo ipo haja ya kufikiri kwa kina, hasa kwenye kukuzalia matunda yake. Yanaweza yakawa matunda mazuri au mabaya.

Na siamini kama kuna mtu anatamani kupata hasara  katika maisha yake, kama hakuna kwanini uendelee kufanya kitu ambacho unaiona hasara yake kabla hata hujaipata?

Leo nakuacha na fikiri hii kwa unachofanya leo, iwe ni fikiri ya kubadilisha tabia yako, iwe ni fikiri ya kubadilisha kile ulikuwa unafanya na hakifai mbele za Mungu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081