Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo, habari za Leo, Mungu ni mwema ametupa nafasi nyingine ya kuiona siku ya leo.

Kufikiri ni jambo la muhimu sana katika maisha yetu, bila kukaa na kutenga muda wako wa kufikiri juu ya maisha yako. Utakuwa unaishi ilimradi siku ziende bila kujua unakoelekea.

Tunaweza tukawa hodari kulalamika kuwa hatuna kianzio cha kuanzisha kitu tunachokitamani, ambacho kitakuwa kinatupa kipato cha kila siku, au kitakuwa msaada kwetu.

Kulalamika huko sio kana kwamba hatupati hata shilingi, kipo kiasi tunapata kwa siku au kwa wiki au kwa mwezi.

Kiasi tunachopata tunaweza kukidharau na kukiona kidogo sana, lakini kiasi kile kile ukikiwekea mipango mizuri unaweza ukapata kitu kizuri baadaye.

Waswahili wakasema “Haba na haba hujaza kibaba” kidogo kidogo mwisho wake huwa kitu kinakuwa kikubwa sana.

Hebu fikiri kila siku unayoamka ukawa unajiwekea shilingi 1,000/= hii ukawa unaiweka kwa uaminifu bila kuigusa.

Ukichukua hicho kiasi kwa siku 365 ambao ni mwaka mmoja utakuwa na shilingi 365,000/= kwa kuwa una malengo jiwekee miaka 5.

Chukua hicho kiasi cha mwaka mmoja cha shilingi  365,000/= zidisha kwa miaka 5, itakuwa ni sawa na shilingi 1,825,000/=

Kinaonekana ni kama kiasi kidogo sana ila ni kikubwa sana kwa mtu ambaye ameamua kuacha kulalamika.

Mtu ambaye ameamua aache kusumbuana na ndugu wampe mtaji, au wamwazime pesa ya kufanya jambo fulani analolitamani kulifanya katika maisha yake.

Kwa mazingira yetu na kwa makuzi yetu linaweza kuonekana ni zoezi gumu sana, na huenda umejaribu mara nyingi na umejikuta unakula Akiba yote uliyojiwekea.

Pamoja na hayo hupaswi kukata tamaa, rudia tena na iweke akiba yako mahali ambapo sio rahisi kwako kuichukua/kuigusa.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com