Haleluya,

Unapaswa kuelewa na kuliweka moyoni hili, hatujaokoka kwa bahati mbaya. Na kama tuliingia kwa bahati mbaya basi sehemu tuliyoingia ni salama kabisa na hatupaswi kutoka.

Mungu anawatazama kwa jicho lake kuu, wale wote waliompokea yeye kama Bwana na Mwokozi wao. Ni neema iliyoje kupata fursa kutoka kwa Mungu inayotulinda usiku na mchana.

Ndio maana unaona Mungu anakuepusha na mambo mengi ya hatari, unabaki unashangaa na kujiuliza imekuwaje Mungu kukuepusha na jambo ambalo kwa akili za kibinadamu lisingewezekana kuepukika.

Ndugu/rafiki yangu, tunalindwa na Mungu, kuokoka kwetu kumefanya Mungu wetu aweke makazi yake kwetu. Ni raha iliyoje kulindwa na Baba yetu aliye mbinguni.

Rejea: Tazama, jicho la BWANA li kwao wamchao, Wazingojeao fadhili zake. ZABURI 33:18 SUV.

Umeona huo mstari, unathibitisha haya ninayokuambia hapa kuwa jicho la Bwana li juu yetu, usiku na mchana Mungu wetu anahakikisha tupo salama.

Ooh Haleluya, tena Neno la Mungu linasema malaika wa Bwana hufanya kituo kwetu tumchao Bwana. Unataka Mungu akufanyie nini ikiwa amejenga uhusiano wetu na yeye, huenda kuna wakati mwingine tumeishia kujiona Mungu hayupo pamoja nasi ila tufahamu yu pamoja nasi.

Rejea: Malaika wa BWANA hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa. ZABURI 34:7 SUV.

Nasikia nguvu mpya kuendelea kumpenda Mungu zaidi na zaidi, kumbe aliyeokoka ana ulinzi wa kutosha kiasi hichi. Nakwambia una ulinzi mkubwa zaidi ya rais/mfalme wa nchi.

Tena Bwana anawasikiliza wenye haki haraka, wenye haki hao ni wale walioamua kuacha dhambi na kuishi maisha matakatifu. Neno la Mungu linasema hivi;

Rejea: Macho ya BWANA huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao. ZABURI 34:15 SUV.

Kama Bwana anaweza kukusikiliza wewe kilio chako, una mashaka gani pale unapokuwa na jambo gumu linalokukabili. Unapaswa kuondoa wasiwasi maana Mungu yu pamoja nawe, sikio lake husikiza wenye haki wake.

Tena Bwana anasema yu karibu zaidi na wale waliovunjika moyo, yaani pale unapojikuta moyo wako umejeruhiwa na makwazo mbalimbali, pale unapojikua umepigwa na changamoto ngumu, pale unapojikuta umeona maisha ndio basi tena. Yeye Bwana huwa karibu nawe kukutia moyo, si umewahi jikuta ulikuwa umevunjika moyo sana ila ghafla ukasikia faraja ya moyo wako inakujia kwa nguvu sana.

Fahamu Roho Mtakatifu amehusika kukusaidia kukuondoa kwenye huzuni yako, na kukupa amani ya moyo wako. Unaweza kupata amani baada ya kusoma Neno la Mungu, unaweza kupata amani baada ya kusikia mafundisho, unaweza kupata amani baada ya kusikia nyimbo za injili, na unaweza kupata amani ya moyo baada ya kusikia shuhuda mbalimbali.

Rejea: BWANA yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa. Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini BWANA humponya nayo yote. ZABURI 34:18‭-‬19 SUV.

Bila shaka umeona nafasi aliyokupa Bwana juu yake, unaweza kuondoka kwenye utumwa wa unyonge sasa ili kutembea katika ujasiri mkubwa mbele za Mungu.

Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu.
www.chapeotz.com
+255759808081.