
Vipo vitu unaweza usielewe chochote na ukabakia kulalamika, na kuona unasemwa vibaya, ama ukaona mtu fulani anasemwa vibaya, au hakupaswa kukemewa hadharani.
Unaona kabisa hakupaswa mtu yule kusema hayo maneno, ukaenda mbali zaidi na kuona watumishi wa Mungu huwa hawapo hivyo.
Mawazo yetu bila kufahamu neno la Mungu linasemaje, yanaweza yasiwe sawa kabisa. Yanakuwa ni mawazo ambayo hayana kitu cha kuyaelekeza katika mwelekeo sahihi.
Ikiwa tunaingiza hekima za kidunia bila kuwa na neno la Mungu mioyoni mwetu, ama bila kuwa na mafundisho sahihi.
Tujue ipo shida, kwa sababu gani ipo shida? Kwa sababu tunafikiri vitu ambavyo vipo wazi kimaandiko alafu tunavipinga.
Mtu anaweza akapata habari mbaya juu ya mpendwa mwenzake, au ndugu yake, au jirani yake, na mtu huyo aliyepata hizo habari akawa ameokoka. Uhusiano wake na Mungu upo vizuri, usifikiri hiyo habari inaweza ikawa ya kawaida kwake.
Habari hiyo inaweza ikaibua hasira ya kiMungu ndani yake, akaikemea kwa nguvu. Asiyeelewa anaweza kufikiri bado hajamjua Mungu sawasawa, au bado hajaokoka sawasawa.
Lakini kwenye Biblia ni tofauti na mitazamo yetu, hili tunaliona kwa Sauli. Baada ya kuletewa habari mbaya, hizo habari ziliibua hasira ya Mungu ndani yake.
Rejea: Na roho ya Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, hapo alipoyasikia maneno yale, na hasira yake ikawaka sana. 1 SAM. 11:6 SUV.
Ukiwa kama mtumishi wa Mungu, unaweza kupata habari ambayo sio nzuri. Na habari hiyo inawahusu watu wako wa karibu, itakuwa ngumu kubaki kwenye hali yako ya kawaida.
Hasira ya Mungu inaweza kuwaka ndani yako, watu wakachukulia ni hasira zako binafsi. Kumbe ni za kiMungu, na zinakutaka uchukue hatua utakayoelekezwa na Roho Mtakatifu.
Hasira hizo zikakupa nguvu na ujasiri wa kusimama mstari wa mbele kukemea na kuonya bila kuona haya kwa mtu yeyote.
Kufanya hivyo kukaleta uponyaji mkubwa sana, uponyaji ambao utakuwa msaada kwa wale walioumizwa.
Uponyaji ambao utawaponya wale ambao walianza kwenda kinyume na maadili ya kiMungu vile yanavyosema.
Tufahamu kwamba sio kila hasira kwa mtumishi wake ni ya Shetani, hasira zingine ni za kiMungu ndani yake. Hasa anapoona uchafu fulani unatendeka alafu hukemewi na mtu.
Mungu akubariki sana.
Samson Ernest
www.chapeotz.com
+255 759 80 80 81