Unaweza ukawa unatamani mtu mmoja aliyekufa kabisa na watu wote wanamjua, na siku anakufa walimwona na walimzika wenyewe.

Ukawa unatamani afufuke tena aje aeleze faida ya kuokoka ukiwa hai, na hasara ya kukataa kuokoka ukiwa hai.

Unaweza ukawa unatamani labda ufe, alafu uje urudi tena uwaeleze watu ubaya wa jehanamu, na uje uwaeleze uzuri wa peponi.

Inawezekana unafikiri hivyo kutokana na umefika mahali umechoka kuwahubiri watu waache kufanya dhambi. Lakini unashangaa wanaendelea kufanya dhambi zaidi bila hofu yeyote.

Unaweza kufikiri huenda akija mtu aliyekufa, anaweza kueleweka haraka kuliko wewe ambaye upo hai, na anaweza akawa na utiisho fulani wa kuwafanya watu waokoke haraka.

Nakwambia unawaza hivyo ila inaweza isiwe kama uwazavyo wewe, kwanini isiwezekane? Kwa sababu asiyetaka kukuelewa wewe mtumishi wa Mungu uliye hai, hata akija mtu aliyekufa hawatamwelewa vile vile.

Tena wanaweza kubadilisha maneno na kusema hakuwa amekufa, bali alikuwa amefishwa mahali sasa ameachiwa mahali alikuwa amefishwa.

Wakati Lazaro ameingia maisha ya furaha ya milele, tajiri yake alivyokufa yeye aliingia kwenye maisha ya mateso. Wakati anamwambia Ibrahim amwambie Lazaro amletee maji kwa kuchovya kwa kidole chake, alivyomwambia haiwezakani alibadilisha mawazo.

Yule tajiri alimwambia Ibrahim amtume Lazaro akawaambie ndugu zake watano waliopo Duniani, kuhusu ubaya wa dhambi. Ili wajue matokeo ya dhambi ni jehanamu, na hali halisi aliyoiona mwenyewe.

Sikia Ibrahim alichomjibu tajiri huyu;

Rejea: Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu, kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso. Ibrahimu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao. Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu. Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu. LK. 16:27‭-‬31 SUV.

Umeona hapo, huo ndio ukweli, kama mtu hataki kuokoka kwa injili inayochapwa na watumishi wa Mungu huku Duniani. Usikifikiri akifufuka mtu aliyekufa wataweza kuokoka.

Usikifikiri mengi kuhusu wasiotaka kuokoka, wewe wahubirie habari njema, waeleze ukweli, ili siku mtu ameingia jehanamu akumbuke kuna mtumishi aliniambia niache dhambi nikakataa.

Akumbuke kuna mtumishi aliniambia niache kuabudu sanamu sikumwelewa, akumbuke kuna mtumishi aliniambia niache pombe nikampuuza, akumbuke kuna mtumishi aliniambia niache uzinzi/uasherati nikamwona hajui kitu.

Wakati anakumbuka hayo yote, yupo kwenye moto wa milele anaungua, lakini kufikiri wakifufuka watu waliokufa wataeleweka zaidi. Huko ni kujidanganya mwenyewe.

MUHIMU; je unapenda kukua kiroho kwa kusoma Neno la Mungu? CHAPEO YA WOKOVU ni jibu lako na mwalimu wako, atakakusimamia kuhakikisha unajenga nidhamu ya kusoma Biblia yako katika mtiririko mzuri. Ili uunganishwe kwenye darasa hili linaloendeshwa kwa njia ya whatsApp, tuma ujumbe wako kwenda namba +255759808081, tumia WhatsApp tu kutuma sms yako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com