“Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani”, Mwa 37:3‭-‬4 SUV.

Yakobo alionyesha upendo wake mkubwa kwa mtoto wake Yusufu, upendo huu ulikuwa mzuri sana kwa mtoto, kama mzazi haukuwa na shida yeyote kwake ukiutazama kwa haraka na inafaa mbele za Mungu mzazi kumpenda mtoto wake.

Upendo wa Yakobo kwa Yusufu ulileta shida kwa ndugu zake, chuki kubwa iliinuka kwao kuona Yusufu anapendwa kiasi kwamba hicho wanachokiona kwake, kwao hawakioni kabisa.

Tunaona Yakobo alimtengenezea kanzu nzuri, kanzu hii ndefu yenye mapambo mazuri aliyoipokea Yusufu kutoka kwa baba yake, ilionesha tofauti kubwa na kanzu zingine walizovaa ndugu zake.

Mwenekano wake mzuri ulionyesha wazi heshima aliyopewa Yusufu na baba yake, jambo ambalo liliibua chuki kwa ndugu zake kiasi kwamba hawakuweza kukaa pamoja wazungumze vizuri na ndugu yao.

Wazazi tunayo kazi kubwa sana kwenye malezi, ukweli usiopingika kuna watoto wanaweza kutuingia moyoni kuliko watoto wengine kutokana na tabia zao, wapo watoto wanakuwa watiifu kwa wazazi kupita watoto wengine. Hii inaweza kuwa sababu mojawapo ya mzazi kumpenda mtoto.

Watoto wa mwisho wanaweza wakawa sababu ya kupendwa na wazazi wengi, jambo ambalo linaweza kuleta matatizo kwa watoto wengine. Wengine wanakuwa na mapenzi na watoto wa kwanza.

Jambo hili kwa mzazi/wazazi linaweza likawa gumu kukwepeka, kwa sababu tuna mifano kadhaa ndani ya biblia ya wazazi walionyesha wazi upendo kwa watoto wao, mmojawapo ni Isaka alimpenda sana Esau kwa sababu ya mawindo yake, na Rebeka kumpenda Yakobo.

Miongoni mwa wanafunzi wa Yesu ambaye anadhaniwa kuwa ni Yohana, pia tunaona upendo wa Yesu ulikuwa kwake, aliachiwa maagizo ya kukaa na mama yake Yesu.

“Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake”, Yn 19:26‭-‬27 SUV.

Tujue kuwa ipo hatari ya kuonyesha upendo wako kwa mtoto mmoja, unaweza kumwingiza kwenye matatizo makubwa kwa ndugu zake, akafanyiwa mambo mabaya kutokana na chuki kubwa waliyonayo juu yake.

Mungu akusaidie uweze kufahamu hili, ili ikusaidie namna ya kujizuia kuonyesha upendo wako kwa uwazi, tujitahidi kuwa na usawa kwa watoto pale inapowezekana kufanya hivyo.

Hii haipo kifamilia tu, hata katika uongozi tuwe makini kwa wale tunaowaongoza, tuweke usawa kwa wote, najua kuna watu wanaumiza na inakuwa ngumu kuwapa ukaribu, muhimu kujitahidi kwenda na watu wote.

Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia yako
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255 759 80 80 81