Unapomjua Mungu vizuri, ukaelewa vitu gani hupaswi kushiriki, vitu gani hupaswi kuvila, eneo gani hupaswi kwenda, na watu gani hupaswi kushirikiana nao kwa mambo fulani wanayoyafanya.
Misimamo yako inaweza kukuletea faida kubwa sana mbele za Mungu, ila mbele za wanadamu inaweza Kukuletea shida kubwa mno. Usipokuwa makini unaweza kuanza kujutia wokovu wako.
Wakati mtu aliyejua thamani ya wokovu wake, hawezi kulalamika pale anapokutana na changamoto kwenye wokovu wake. Mtu yeyote aliyemjua vizuri anayemwabudu, anayemwamini, anayempelekea shida zake, mtu huyo hawezi kujuta pale anapokutana na mapingamizi mazito kwenye imani yake.
Mtu anayefika mahali anaanza kutamani kurudi nyuma, kwa sababu amekutana na mambo magumu katika ukristo wake. Mtu huyo atakuwa hajajua vizuri yule anayemwabudu, atakuwa hajajua vizuri kwanini ameokoka.
Walio na imani thabiti kwa Mungu wao, hawawezi kutishwa na mazingira, hawawezi kujutia wokovu wao kwa sababu yeyote ile. Hata kama watakutana na vitisho vizito sana mbele yao, bado wataendelea kusimama vile vile na Yesu wao.
Hili tunajifunza kwa watumishi wa Mungu, Shedrack, Meshack, na Abednego, wanatufundisha kusimamia misimamo yetu ya imani kisawasawa kwa Mungu wetu. Yasiwepo mazingira yakatufanya tukamkataa Mungu wetu, na kugeukia miungu mingine kwa sababu tu ya matisho ya wakuu wenye mamlaka.
Kitu kingine tunachokiona kwenye hili la akina Shedrack, Meshack, na Abednego, baada ya kukataa kuabudu sanamu ya mfalme Nebukadreza aliyoagiza kila mmoja aisujudu. Wapo watu waliowaona wamekaidi agizo la mfalme, wakapeleka habari haraka za mashtaka kwa mfalme Nebukadreza.
Rejea: Wewe, Ee mfalme, ulitoa amri ya kwamba kila mtu atakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, ni lazima aanguke na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu; na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa katika tanuru ya moto uwakao. Wako Wayahudi kadha wa kadha uliowaweka juu ya mambo ya wilaya ya Babeli, yaani, Shadraka, na Meshaki, na Abednego; watu hawa, Ee mfalme, hawakukujali wewe; hawaitumikii miungu yako, wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha. DAN. 3:10-12 SUV.
Tunajifunza nini hapa, katika maisha yetu ya imani, tunaweza kukutana na mazingira kama ya akina Shedrack, Meshack, na Abednego. Lakini pamoja na kukutana na mazingira magumu kama hayo, hatupaswi kuacha imani zetu.
Tutafika mahali tutapelekewa hati za mashtaka kwa wakuu wenye mamlaka ya nchi, ila hilo lisitufanye tukaacha imani zetu. Hilo lisitufanye tukakana imani zetu mbele za watu, hiyo itakuwa ni aibu yako.
Tunapaswa kusimama vile vile na imani zetu, haijalishi mazingira yanatutaka tusionyeshe ukristo wetu. Hilo lisitusumbue, tunapaswa kushikilia imani zetu mpaka dakika ya mwisho.
Tunaona kulikuwepo na adhabu ya kutupiwa kwenye tanuru la moto kwa wale wote ambao wangekiuka agizo la mfalme. Hawa watumishi wa Mungu hawakuwa wakibahatisha, tunaona waliitwa mbele ya mfalme Nebukadreza ila waliendelea kuonyesha msimamo wao mbele ya mfalme.
Mashtaka yatakuja mengi kwenye huduma yako ila hakikisha hutotelewi kwenye imani yako, hakikisha hutotelewi kwenye msimamo wako wa kuendelea kumpenda na kumtumikia Yesu Kristo.
Leo unaweza usilazimishwe kuabudu sanamu ila ukalazimishwa kutoa rushwa ya ngono ili kupata kazi. Usikubali kuzalilisha ukristo wako kwa kitu ambacho kipo ndani ya uwezo wa Mungu unayemwabudu.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
chapeo@chapeotz.com
www.chapeotz.com
+255759808081