Miaka ya nyuma kabla sijapata somo hili, niliweka matumaini makubwa sana kwa ndugu na rafiki. Pale ndugu aliposhindwa kunisaidia kile nilikuwa nahitaji kutoka kwake, ilinifanya nipate uchungu mwingi sana moyoni. Na wakati mwingine kumchukia kabisa kwa kumwona hana msaada wowote kwangu.

Baada ya kupitia katika changamoto hiyo miaka hiyo ya nyuma, kuna somo/funzo kubwa sana niliondoka nalo. Funzo hili lilinifanya niache kumtegemea mtu kwa asilimia zote, tena nilivyopata neema ya wokovu ndio ilinifanya niwe imara zaidi.

Nilichojifunza hata kama namdai mtu na ameniahidi kunilipa leo hii, sitaweka asilimia zangu zote katika kulipwa hilo deni. Na kama kuna mtu aliniomba pesa sitamwahidi kumpa kwa kutegemea pesa ya deni.

Ilinifunza pia nikiwa na shida na pesa, alafu nikamwomba mtu anisaidie kiasi ninachotaka. Sitamtegemea kunipa kwa asilimia zote pale anaponiahidi kunipa hicho kiasi, na nimeona mara nyingi wakikwama kunipa hicho kiasi, na nimekuwa siumii sana kwa hilo.

Kutomtegemea sana mtu, imekuwa ikiniepusha sana na maumivu yasiyo ya lazima, zaidi nimekuwa naondoka na somo kubwa. Na wakati mwingine nimekuwa nikisitisha ombi langu na kuona huenda huo msaada ungekuja kunipa shida mbeleni.

Hayo ni maisha ya kawaida kabisa ya kimwili na wengi tunakutakana nayo, nimekueleza hayo kukupa mwanga kwa hili ninaloenda kukueleza hapa.

Mara nyingi sana tumekuwa tunategemea ndugu zetu, wazazi wetu, na rafiki zetu, watufanyie mambo fulani katika maisha yetu. Badala yake tumekuwa hatupati huo msaada, na tumeishia kuwachukia na kujitengeneze uchungu ambao umekuwa mgumu kuachilia na kusamehe.

Wakati mwingine tumeacha kumtegemea Mungu wetu na kutegemea binadamu wenzetu. Badala yake tumeishia kulaumu na kuwaona vile tunavyowaona.

Rejea: Macho yetu yamechoka Kwa kuutazamia bure msaada wetu; Katika kungoja kwetu tumengojea taifa Lisiloweza kutuokoa. OMB. 4:17 SUV.

Hawa ndugu walitazamia kupata msaada kutoka kwa taifa lingine, badala yake waliishia kusubiri bila mafanikio yeyote.

Hapa tunapata kujifunza kwamba, wa kutegemea kwa asilimia zote ni Mungu pekee na si mwanadamu mwenzako. Mungu hawezi kukuangusha ukimtegemea, Mungu hawezi kukusaliti ukimtegemea, na Mungu hawezi kukuzalilisha kwa watu akikusaidia.

Nguvu zako nyingi unapaswa uzielekeze kwa Mungu wako, acha kabisa mawazo ya kumtegemea mwanadamu atakusaidia. Leo mnaweza kuwa rafiki, kesho akakugeuka/kukukataa kabisa.

Yatoe maisha yako yote kumtegemea Mungu wako, kumtegemea Mungu hakukuondolei uhusiano wako na watu. Bali inakujengea mazingira mazuri ya kuepuka kujenga chuki na fulani, kwa sababu hajakusaidia kile ulikuwa unataka.

Mungu akubariki sana.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081