Ukiwa na uhakika kesho ukiamka asubuhi una fedha ya kutosha ya kutumia bila tatizo lolote, na ukiwa na uhakika fedha uliyonayo inaweza kukufikisha miezi kadhaa bila tatizo. Unakuwa na amani sana na utulivu mzuri moyoni mwako.

Uhakika ukiwepo ndani yako kuwa unalindwa na nguvu za Mungu, hata kama kitokee kitisho chochote kile cha nguvu za giza, huwezi kuwa na hofu yeyote.

Kama una uhakika na kazi uliyonayo inaweza kukupatia fedha ambayo itaweza kukupa mahitaji yako ya msingi, utakuwa unafanya kazi ukiwa na uhakika.

Ikitokea kazi unayofanya haikupi fedha ambazo unaweza kujikimu vizuri kimaisha, kazi hiyo utakuwa unaifanya. Lakini ndani yako utakuwa huifurahii sana kutokana na kuwa na mawazo mengi.

Unapokuwa umeokoka na ukapata uhakika kuwa Mungu hakuhesabii dhambi zako tena, unakuwa na ujasiri mkubwa ndani yako na mbele za watu, ila unapokosa uhakika wa kusahemewa dhambi zako unakuwa unaishi maisha ya hofu nyingi.

Hujawahi kuona mtu ameokoka kabisa ila bado anashindwa kufanya vitu vizuri vya kumtukuza Bwana, hii ni kutokana na kujiona bado ana hatia mbele za Mungu.

Anaona akimtumikia Mungu watu watamwonaje na wakati alikuwa yupo pamoja nao kwenye maisha ya dhambi, maisha ambayo yalikuwa hayatamaniki mbele za Mungu.

Tofauti na mtu aliyefundishwa akajua kuwa yeye amefanyika kiumbe kipya kabisa, Mungu hakumbuki tena makosa yake, dhambi ambazo Bwana hazihesabii tena.

Rejea: Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao.  Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi. RUM. 4:7‭-‬8 SUV.

Unapaswa kutembea kifua mbele kwa ujasiri mkubwa kwa sababu unao uhakika wa kutokuhesabiwa dhambi zako zote, una heri kubwa sana kwenye maisha yako.

Wakati wengine wanaona heri yao wamezaliwa kwenye familia nzuri zenye uwezo mkubwa kifedha, wakati wengine wanaona heri yao wamesoma shule nzuri ya kiwango.

Wakati wengine wanaona heri yao wamejenga nyumba nzuri za kuishi, wakati wengine wanaona heri yao wamepata kazi nzuri sana zenye mshahara mkubwa.

Wewe jivunie uheri wako wa kusahemewa dhambi zako zote, na Mungu anakuwa hazikumbuki tena hizo dhambi, maana ameshakusamehe makosa yako yote mabaya uliyoyatenda.

Labda yule ambaye hajaokoka, ambaye bado anafanya mambo mabaya ya kumkosea Mungu, huyo hana heri, bali Mungu anamhesabia mwenye dhambi.

Kama umeokoka na Yesu Kristo amefanyika Bwana na mwokozi wa maisha yako, heri yako ndugu yangu, furahia na endelea kutunza maisha yako ya wokovu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com