Kama ulikuwa unafikiri unaweza kuyamaliza makwazo au unaweza kuepukana nayo, utakuwa unajihangaisha bure. Maana unachokihangaikia kukikwepa hakina budi kuja kwako, japo unaweza kukaa mbali na wenye makwazo.

Kukaa mbali na watu wanaopenda kuleta makwazo, inaweza ikawa njia nzuri kwa muda ila unaweza kukutana na makwazo kwa namna ya tofauti kabisa kupitia hao hao uliowakwepa au watu wengine kabisa.

Ukiwa nyumbani kwako/kwenu unaweza kukutana na makwazo mengi tu ila hupaswi kuwa mtu uliyejaa jazba kila wakati, hasira haipaswi kukaa kifuani mwako kwa sababu ya makwazo unayokutana nayo.

Makwazo yanaweza kuletwa na watoto wako uliowazaa kabisa, makwazo yanaweza kuletwa na baba/mama yako, makwazo yanaweza kuletwa na mke/mume wako, makwazo yanaweza kuletwa na ndugu zako, makwazo yanaweza kuletwa na wafanyakazi wenzako, makwazo yanaweza kuletwa na wanafunzi wenzako.

Unaweza kuona vile huwezi kuepukana na hili la makwazo, hata kama wewe hupendi kumkwaza mtu, unaweza kumkwaza kwa namna ambayo hukujua kama umeleta makwazo kwake.

Unaweza kumkwaza mtu vile umesimama vizuri kwenye msimamo wako, vile unamcha Mungu vizuri, vile mwaminifu mbele za Mungu, vile mwaminifu kwa vitu vya wengine, vile mwaminifu kwenye ndoa yako. Yupo mtu mwenye tabia chafu anakuwa anakwazika anapokuona upo vizuri kwenye maeneo hayo niliyokutajia hapo.

Makwazo ya namna hiyo hayawezi kuleta madhara yeyote kwa mtu wa Mungu, kama mtu anakuwa anakwazika kwa sababu ya mambo mazuri anayofanya mtu, ama kwa sababu mtu ni mwaminifu mbele za Mungu. Huyo anayekwazika anahitaji msaada mkubwa mbele za Mungu.

Biblia inaonya wale ambao wanakuwa vishabishi au waletaji wa makwazo kwa watu wema, sio yale makwazo ambayo mtu anakuwa anakwazika baada ya kuona mtu amefanikiwa kwenye eneo fulani. Hayo sio makwazo yenye mashiko.

Rejea: Akawaambia wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake! LK. 17:1 SUV.

Pamoja na tumeona kuwa hatuwezi kukwepa makwazo, Neno la Mungu linaonya wale wanaoleta/wanaosababisha hayo makwazo yaje. Ni ngumu kukwepa hili ila jitahidi usiwe sehemu ya makwazo kwa makusudi, tuache ile unamkwaza mtu bila wewe kujua. Pale tunajua, tujitahidi kuepuka tusiwe sehemu ya makwazo kwa wengine.

Umekuwa sehemu kubwa ya kuleta makwazo kwa watu, achana na hiyo tabia mbaya mara moja, maana ni tabia ya watu wasiomjua Kristo. Walio na Roho Mtakatifu ndani yao hawawezi kuwa sehemu ya makwazo, tena yale makwazo ya kukusudia kabisa.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com
+255759808081