Cheko za watu wengi ni feki, wengi wanalia, mioyo yao imejaa machozi mengi, wengi usiku hawapati usingizi mzuri kwa sababu ya msongo wa mawazo. Lakini ukimwona mchana uso wake una kicheko cha kulazimisha, ukimuuliza ndugu vipi, atakuambia shwari kabisa.

Shwari mdomoni ila moyoni mwake kumejaa huzuni, anayo maumivu makali yasiyokoma moyoni mwake, ukweli hataki kusema labda kwa sababu hataki kuonekana dhaifu, labda kwa sababu ni mtu mzima hataki watoto wake waone mama/baba yao analia machozi.

Yupo mama amejaa huzuni nyingi kwa kukosa mtoto wa kumzaa yeye, miaka mingi imepita akitafuta mtoto, ndani yake amefika mahali anajisikia huzuni tu. Anapoona wanawake wengine wakinyonyesha watoto wao, ndani yake ni kama anatoneshwa kidonda.

Yupo binti ambaye anaendea kutoka kwenye umri wa ubinti, haoni dalili ya kupata mume wa kumwoa, ndani yake amejaa huzuni nyingi na maumivu makali anapoona wadogo zake wanaolewa yeye anaachwa yupo vile vile.

Mwingine hajui afanyaje, kazi aliyokuwa nayo ameachishwa hajui afanyeje, ndani mwake anayo huzuni nyingi na maumivu makali anayoopitia kwenye maisha yake. Huenda hata kula yenyewe imekuwa tabu kubwa kwake, lakini mtu huyu huenda anajikausha mbele za watu.

Kuna mtu anapitia mambo magumu kwenye ndoa yake, anayo huzuni nyingi sana ndani ya moyo wake, akiona wenzake wanavyopendana moyoni mwake anakuwa kama anatoneshwa kidonda kinachompa maumivu makali.

Lakini akiwa kwa watu anaficha hiyo hali kana kwamba hali ni shwari ila moyoni kwake amebeba mzigo mzito sana, ni vile tu hataki kuweka mambo wazi kwa watu wanaoweza kumsaidia ushauri.

Wengine hadi mbele za Mungu huwa hawajiweki wazi sana, akienda mbele za Mungu kuomba anakuwa anapitapita pembeni bila kumweleza Mungu amwondolee mzigo mzito alionao.

Leo maandiko matakatifu yanatuonyesha wazi kuwa kuna wakati mtu anaweza kuweka wazi ukweli wake kuhusu huzuni yake aliyonayo na maumivu makali aliyonayo moyoni mwake.

Rejea: Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu, ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu. RUM. 9:1‭-‬2 SUV.

Zipo nyakati zisizoelezeka hata kwa watu, maana unaona kabisa ukiwaambia watu hawatakuelewa, pamoja na hayo usikae na huzuni nyingi na maumivu makali moyoni mwako.

Kukaa na huzuni nyingi muda mrefu bila kuitoa mahali popote, kukaa na huzuni ambayo imezalisha maumivu makali, kwa sababu ya kujificha usionekane mtu dhaifu. Huko ni kujiumiza bila sababu, utafika mahali utaanza kufikiri mambo mabaya.

Wakati ungemweleza Mungu kwa uwazi kabisa, huo mzingo usingekuzidia, bali ungemtwisha mwenye mzigo, utasema kama ni kuomba umeomba sana lakini bado huoni majibu ya maombi yako.

Maandiko yanatuasa tuombe pasipo kukoma, kwa kuwa huna Neno la Mungu la kutosha huenda umechoka na kukosa matumaini kabisa, umebaki mtu wa huzuni, mtu usiye na tumaini lolote juu ya maisha yako.

Iweke wazi huzuni yako na maumivu yako makali, mweleze ndugu yako katika Kristo unayemwamini, mweleze vile unajisikia, anao uwezo wa kukushauri na kukuombea. Umeona hilo ni gumu kwako nenda mbele za Mungu ukajieleza kwa uwazi kabisa.

Sema kweli katika Kristo, wala usiseme uongo, usiseme hali ni shwari huku unajua huzuni uliyonayo ni kubwa, usiseme unayo amani wakati moyoni mwako kuna furushi la maumivu makali. Huenda hayo maumivu yamekusababisha presha, kama sio presha ni vidonda vya tumbo.

Tumesoma andiko takatifu hapo juu linaonyesha vile mtume Paulo alijiweka wazi, akasema vile anavyojisikia, tena akasema hataongea uongo, jiulize ni mara ngapi umejifariji unayo amani/furaha wakati unayo huzuni nyingi na maumivu makali moyoni mwako.

Usijidanganye mwenyewe, hakikisha unapata furaha ya kweli kutoka kwa Yesu Kristo mwenyewe, mwambie akurejeshee furaha yako leo. Naye atakurejeshea maana Mungu wetu ni mwaminifu kwetu, hutujibu maombi yetu.

Kama bado hujajiunga na kundi letu la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, tuma ujumbe wako kwa wasap namba 0759808081 wenye neno CHAPEO YA WOKOVU utaunganishwa.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081