“Hata Simoni alipoona ya kuwa watu wanapewa Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono ya mitume, akataka kuwapa fedha akisema, Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu. Huna fungu wala huna sehemu katika jambo hili, kwa kuwa moyo wako si mnyofu mbele za Mungu”, Mdo 8:18‭-‬19‭, ‬21 SUV.

Tunaweza kutishwa na nguvu kichawi, tunaweza kuona wachawi au waganga wa kienyeji wana nguvu nyingi kuliko watu wengine, nikuambie haya ni mawazo yetu na bado hatujajua uweza wa nguvu iliopo kwa Roho Mtakatifu.

Ukifuatilia vizuri kitabu chote cha matendo ya mitume utaona waliopata ubatizo wa Roho Mtakatifu ni wale waamini au wanafunzi walipojikabidhi mbele za Mungu sawasawa.

Simoni ambaye alikuwa mchawi mkubwa na aliyeaminiwa sana kwa miujiza yake, alifika mahali nguvu hizo zilipelea na akatamani kununua nguvu na kipawa cha Roho Mtakatifu. Lakini alikataliwa na Mungu kwa sababu moyo wake haukuwa ukimwelekea yeye.

“Nipeni na mimi uwezo huu, ili kila mtu nitakayemweka mikono yangu, apokee Roho Mtakatifu. Lakini Petro akamwambia, Fedha yako na ipotelee mbali pamoja nawe, kwa kuwa umedhania ya kuwa karama ya Mungu yapatikana kwa mali”, Mdo 8:19‭-‬20 SUV.

Moja ya nguvu inayotamaniwa sana na wachawi na waganga wa kienyeji ni hii nguvu ya Roho Mtakatifu, hii nguvu inazidi ya kwao, ndio maana wanaitaka ili waitumie katika mambo yao ya giza.

Habari mbaya kwao ni kwamba hawawezi kuipokea kwa sababu ya matendo yao maovu, hadi pale watakapoamua kumpa Yesu maisha yao kwa kuacha uovu wao na kuamua kutenda yaliyo mema.

Tunaona hata kwa wafuasi wa Yesu kabla ya siku ya Pentekoste, walijikabidhi kwa Bwana wao aliyefufuka na kudumu katika maombi, wakiingoja ile ahadi ya Roho Mtakatifu.

Hiyo haikutosha, waliishi katika maisha ya kujitenga mbali na dhambi na kutii yale mafundisho ya mitume, jambo ambalo kwa mtu mwovu hatamani kuyaacha hayo maisha. Lakini anakuwa anatamani nguvu ya Roho Mtakatifu iwe kwake.

Tendo hili jema na kubwa la kujazwa Roho Mtakatifu lilitokea kwa mara ya kwanza kwa waamini waliomgeukia Yesu na kuziacha njia zao mbaya, na kuishi maisha yanayompendeza na kumtii Kristo.

“Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali”, Mdo 2:42 SUV.

Roho Mtakatifu hamjazi kila mtu isipokuwa kwa yule anayeenenda kwa Roho pamoja na kuongozwa naye, ndio sharti la kujazwa Roho.

“Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho”, Efe 5:18 SUV.

Ukiona muujiza wowote ukitendeka kwa kudhani ni kwa sababu ya mtu amebatizwa na Roho, alafu huyo mtu matendo yake mbele za Mungu yakawa mabaya, anatenda dhambi, ujue mtu huyo hajabatizwa na Roho Mtakatifu.

Akionyesha amejazwa na Nguvu za Roho Mtakatifu na kuonyesha miujiza mbalimbali huku anatenda dhambi, ujue huo ni ujazo mwingine wa nguvu za kipepo na sio wa Roho wa Mungu.

“Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”, Mt 7:22‭-‬23 SUV.

Usije ukamwona mtu anayejiita mtumishi wa Mungu akitenda matendo ya miujiza kupitia jina la Yesu, huku anafanya matendo maovu, ukasema huyo ni mtumishi wa kweli wa Mungu.

Miujiza sio uthibitisho wa mtu kuwa mtumishi wa Mungu wa kweli, miujiza mingine inatokatana na nguvu za kipepo, ambayo haitokani na nguvu za Mungu.

Mtu akimtamani Roho Mtakatifu sharti maisha yake ayakabidhi mbele za Mungu, amkiri Kristo na kuyaishi maisha yanayompendeza Yeye kila wakati, hapo ataweza kuipokea hii nguvu ya Roho.

Waliopata neema hii ya kupokea uweza na nguvu za Roho Mtakatifu hawapaswi kuwa na mashaka yeyote, ukimwona mtu ana mashaka juu ya uwezo wa Roho Mtakatifu ujue ni uchanga wa kiroho na kutokujua kile amebeba.

Soma neno ukue kiroho
Liwe jua iwe mvua soma biblia
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081