
Tukisema kila mmoja wetu aseme mahitaji yake, kuna mahitaji utayasikia mpaka utahisi kuishiwa pumzi kutokana na mambo ambayo watu wanayo mioyoni mwao.
Kila mmoja analo hitaji lake muhimu sana, anapambana usiku na mchana kuhakikisha analipata hitaji la moyo wake. Hili sio jambo geni sana kwa kila mtu, hata wewe unayesoma ujumbe huu, inawezekana kabisa una hitaji la muhimu sana. Ambalo unalihitaji Mungu akutendee katika maisha yako au katika familia yako.
Inawezekana wapo pia wamefika kipindi wamevunjika mioyo yao baada ya kuona hawajibiwa maombi yao, huenda wapo wengine wameacha na wokovu kabisa baada ya kuchelewa kujibiwa maombi yao.
Wapo wameomba sana juu ya waume/wake zao wawabadilishe tabia zao, wakasubiri Mungu awabadilishe tabia fulani mbaya, badala ya kubadilika wamekuwa zaidi ya awali. Yaani kama vile maombi yao yamechochea waelendelee kufanya mambo machafu.
Wapo wazazi wameomba sana juu ya watoto wao, lakini pamoja na kuomba sana, hakuna matokeo mazuri waliyoyaona kuhusu watoto wao. Baadhi ya wazazi wamefika kipindi wakavunjika mioyo yao, hawana tena hamu ya kuendelea kumweleza Mungu juu ya hitaji lao.
Kuchoka huko ni ishara kwamba watu hawa wamekosa Neno la Mungu ndani yao, mtu aliye na Neno la Mungu ndani ya moyo wake. Mtu huyo anajua Mungu anayemwomba na anayemwamini, anajibu kwa wakati wake sahihi.
Tena anajua Mungu anataka nini kabla hujaenda mbele zake, na mtu anapoenda mbele zake anapaswa kuomba kupitia jina lipi. Sharti uombe kwa jina la Yesu Kristo, ndipo atakusikia na kukujibu haja ya moyo wako.
Mtu yeyote anayeomba, anapaswa kuomba kwa jina la Yesu Kristo, unapoomba kwa jina la Yesu, lazima alifanye kwa mapenzi yake hilo uliombalo.
Rejea: Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya. YN. 14:14 SUV.
Umeambiwa uombe lolote kwa jina la Yesu Kristo, lo lote, usije ukasema hili labda ni dogo sana halifai kumwomba Mungu. Kama kwa akili zako umefika mwisho, unahitaji msaada wa Mungu.
Yesu mwenyewe ametuhakikishia kupitia Neno lake, kuwa tukiomba neno lolote kwa jina lake, atalifanya. Kama ni hivyo kwanini uwe na wasiwasi kuhusu maombi yako mbele za Mungu.
Una jambo zito limesimama kama ukuta kwenye familia yako, kwenye kazi yako, kwenye biashara yako, kwenye kampuni yako, kwenye ndoa yako, kwenye masomo yako. Nenda mbele za Mungu uombe, utaona Mungu akilifanya lile uliloliomba kwake.
Zingatia sana hili, kama unahitaji Mungu akutendee kile unahitaji kutoka kwake, alafu uhusiano wako na Mungu upo vizuri, na umesamehe wale waliokukosea. Maombi yako lazima yasikiwe na yajibiwe, imani yako inapaswa tu kuwa kwa Yesu Kristo.
Kama unahitaji kujenga tabia mpya ya kusoma Biblia yako kila siku, karibu group la whatsApp la kusoma Neno la Mungu kila siku. Tuma ujumbe wako whatsApp kwenda namba +255759808081.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com