“Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia wale waliomfuata, Amin, nawaambieni, Sijaona imani kubwa namna hii, kwa ye yote katika Israeli”, Mt 8:10 SUV.

Imani ya huyu akida aliyemwendea Yesu amponye mfanyakazi wake ilipita watu wote ambao Yesu aliwakuta katika Israeli, tunaweza kusema alikuwa mtu wa kwanza kumshangaza vile alivyokuwa na imani kubwa.

Imani hii iliunganisha upendo mkuu kwa ajili ya mtu mwingine na tumaini kuu katika Kristo, na mtu huyo aliyekuwa na shida akapokea muujiza wake wa uponyaji kupitia bwana wake.

Habari hii inatufundisha mambo mengi sana, mojawapo ni kuwa tunaweza kupishana na miujiza yetu kutokana na watu wanavyochukulia matatizo yetu kutokana na mtazamo wa dunia hii.

Watu wanaweza kukuambia kwa hilo tatizo hutaweza kupona, fulani alikuwa na hilo tatizo akahangaika huku na kule lakini hakupata msaada hadi akafa.

Ukisikia hivyo unaweza kuzimia moyo na kujiona mtu wa kufa tu, au kujiona hilo ndio tatizo lako la maisha yako yote hadi unakufa.

Tunahitaji kuwa na imani mbele za Mungu wetu, wakati mwingine tunaenda mbele za Mungu ila imani zetu zinatuambia haiwezekani, alafu tunakazana kuomba au tunataka watu watuombee ila sisi wenyewe hatuamini kama Yesu anaweza.

Tukiwa wana wa Mungu tunapaswa kuimarisha imani zetu kupitia neno la Mungu, imani inajengwa kupitia neno la Kristo;

“Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo”, Rum 10:17 SUV.

Inategemeana na wewe unasikia nini sana, unasoma nini sana, ukiwa unasikiliza sana habari zingine nje na mafundisho ya neno la MUNGU, na ukiwa unasoma sana habari zingine nje na neno la MUNGU. Uwe na uhakika imani yako utaijenga kupitia hayo, iwe imani sahihi au siyo sahihi.

Mungu akusaidie imani yako iwe kubwa mbele za Mungu, wakati dunia inaona kushindikana wewe uone kuwezekana kupitia jina la Yesu Kristo.

Soma neno ukue kiroho

Mungu akubariki sana

Samson Ernest

+255759808081