Mtu wa kwanza anayeweza kuzuia muujiza wako, mtu huyo ni wewe mwenyewe, mtu anayeweza kuyafanya mambo yako kuzidi kuwa magumu zaidi, mtu huyo ni wewe mwenyewe.

Upo wakati huwa tunaanza kumtafuta adui wa maisha yetu anayesababisha mambo yetu kushindikana, tunamsahau adui huyo namba moja ni sisi wenyewe, ndio adui anaweza akawa wewe mwenyewe.

Unaposhindwa au unapoacha kuamini kuwa Mungu anaweza kukutoa kwenye shida yako, unakuwa unazuia muujiza wako. Kweli kabisa madktari wamekuambia ugonjwa ulionao hauwezekani kupona, kweli kabisa inaweza kuwa walimu na wanafunzi wenzako wamesema huna akili na matokeo yameonyesha hilo.

Je, wewe baada ya kuambiwa hivyo umeamini huna akili kweli? Je, baada ya kuambiwa huponi huo ugonjwa na wewe umeamini huponi kweli? Kuamini hayo maneno unakuwa umejiwekea ukuta mwenyewe na wakati ulipaswa kufahamu kwamba hakuna linaloshindikana kwa Mungu.

Hili la kuwa na imani kwa Mungu sawasawa lilimfanya Mungu ajivunie Ayubu, Mungu alijua ana mtumishi asiyeweza kumwacha kwa hali yeyote ile. Ayubu alijua uweza wa Mungu, alijua hata kama Dunia nzima itasema haiwezekani, alijua kwa Mungu itawezekana.

Rejea: Ndipo Ayubu akamjibu BWANA, na kusema. Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika. AYU. 42:1‭-‬2 SUV.

Usipojua uweza wa Mungu juu ya maisha yako, utakuwa mhanga wa maisha yako kwa mitazamo ya kibinadamu ilivyokuona wewe ulivyo haiwezekani kuwa kama unavyotamani kuwa. Maana tayari umeondoa nafasi ya Mungu ndani yako kwa kusikiliza majibu ya madaktari, ama walimu wako, ama wazazi wako, ama marafiki zako.

Inawezekana kabisa watu wamesema hutoweza kuishi maisha matakatifu ya kumpendeza Bwana Yesu, kuanzia sasa elewa hayo ni maoni yao ila kwa Mungu inawezekana kabisa kuishi maisha matakatifu ya kumpendeza Yesu Kristo.

Rejea: Yesu akawakazia macho, akawaambia, Kwa wanadamu hilo haliwezekani; bali kwa Mungu yote yawezekana. MT. 19:26 SUV.

Sasa mtumishi mimi nina mwaka wa kumi sasa sina mtoto au ndugu yangu hana mtoto, inawezekana vipi kumpata mtoto? Inawezekana unajiuliza hilo swali ila nikuambie ukweli, kukosa imani mbele za Mungu hadi kufika hatua ya kukata tamaa. Hiyo ndio shida kubwa uliyonayo kuliko hiyo miaka uliyokaa huna mtoto.

Unachotakiwa kufanya kwako ni kugeuza mawazo yako ya kutoamini Mungu anaweza, na kuwa na imani ya kuamini hakuna linaloshindikana kwa Mungu wako.

Utaondoaje sasa mawazo hasi na kuwa na mawazo chanya ya kuamini hakuna linaloshindikana kwa Yesu Kristo? Hilo liko ndani ya uwezo wako maana tayari nimeshakupitisha na naendelea kukupitisha kwenye maandiko matakatifu yanayoonyesha hakuna linaloshindikana kwa Mungu.

Rejea: Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume. Mwanzo 18 :14.

Kazi uliyobaki nayo sasa ni kufanya mazoezi ya kuweka imani yako mbele za Mungu, hata kama Mungu atachelewa kujibu kama ulivyotarajia akujibu. Unapaswa kufahamu kuwa Mungu huwa hachelewi.

Rejea: Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba. 2 Petro 3:9.

Mwisho, yaweke haya kwenye matendo ndipo utaweza kumwona Mungu akitenda mambo makubwa katika maisha yako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
WhatsApp: +255759808081.