“Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu”, Yn 15:20 SUV.

Iwe makusudi au isiwe makusudi jambo hili huwezi kulikwepa ukiwa mwamini, unaweza kujitahidi kutenda mema ila utakutana nalo.

Kuudhiwa itakuwa sehemu yako, kukataliwa, kuchukiwa, kutengwa, kuteswa, kuchekwa, na mengine mengi yanayofanana na hayo, yanaweza kumkuta mwamini kwa ajili ya kumwamini Kristo.

Unaweza kusikia haya ukaogopa na kuona bora ukae bila kumpokea Kristo kuepukana na ghasia hizi nyingi, nitakufananisha na mtu anayeogopa kufanikiwa na kuona bora abaki na umasikini wake asije akakutana na changamoto.

Changamoto zipo na hatupaswi kuziogopa hasa kwenye eneo sahihi unalokuwepo, mambo yanayoweza kutupata waamini hayapaswi kutuzuia kuendelea kumwamini Yesu Kristo.

Tunapaswa kuelewa tukiwa wafuasi wa Yesu hapa duniani tutachukiwa, tutateswa, tutakataliwa na jamaa zetu, wazazi wetu, ndugu zetu kwa ajili ya jina lake.

Hii itupe kuelewa kwamba dunia ni mpinzani mkubwa wa Kristo na watu wake katika kipindi chote cha historia, maana yake sio jambo lililoanza siku za hivi karibuni, wapo watu wamepita kwenye vipindi vigumu hadi sasa kuona kanisa limesimama hivi.

Tunaeleza haya ili wewe mwamini wa kweli uweze kufahamu kuwa dunia ikiwa ni pamoja na taasisi za dini za uongo na makanisa ya uongo, siku zote yatampinga Mungu wa kweli na kanuni za ufalme wake.

Siku zote dunia itaendelea kuwa adui na mtesi wa wale waamini walio waaminifu kwa Mungu wao siku zote hadi wanaondoka hapa duniani ama hadi mwisho wa dunia.

“Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu”, Yak 4:4 SUV.

Sababu nyingine ya waamini kukutana na mateso humu ulimwenguni ni kuwa na msingi tofauti wa imani, matendo yao yanakuwa yanapishana na ulimwengu unavyotaka waishi au waamini.

“”Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia”, Yn 15:19 SUV.

Mienendo safi ya waamini inapopishana na ulimwengu unavyotaka mara nyingi muumini huyu hukutana na nyakati ngumu, nyakati ambazo huwa mateso kwake, hasa zile jamii zilizopotoka.

Kufahamu haya itatusaidia kuelewa nyakati mbalimbali tunazokutana nazo katika maisha yetu, ili tusijione tumekosea njia bali tuone ni hali ya kawaida kwa mwamini, mtu aliye na msimamo wa Kimungu.

Zingatia moyoni kuwa Mungu yupo na wewe siku zote, simama katika imani yako, bila kujalisha dhoruba unazokutana nazo katika maisha yako ya wokovu, kuna wakati utakaso vitu fulani vizuri ambavyo ungevipata vingeharibu kabisa uhusiano wako na Mungu.

Soma neno ukue kiroho
Kwetu kusoma biblia ni maisha
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081