Zipo nafasi ambazo tunakuwepo kwa kuwekwa au kwa kuchaguliwa na kiongozi aliye juu yetu, tunavyofahamu kila kiongozi awe wa kanisa au serikali, anapenda kuwa na watu watakaoendana nao. Ili waweze kumsaidia kutimiza maono aliyonayo katika utumishi/utawala wake.

Kitu ambacho huwa hatukifikiri kabisa ni kuhusu nafasi za uongozi tulizonazo, wapo wengine huwa tunajisahau sana, kujisahau huko huwa hatujiandai sana kuhusu maisha yajayo. Yaani ikitokea umeondolewa kwenye nafasi uliyokuwepo uwe tayari ulishajiweka vizuri, ukiwa ulijiweka vizuri hutokuwa na mshtuko mkubwa.

Kwa kuwa leo tunajifunza kupitia maandiko ya biblia, utaenda kuona ni jinsi gani kiongozi aliyeopo sasa hivi na wewe ni miongoni mwa watendaji kazi wake. Unapaswa kujipima kwa kujihoji hili jambo, na unapaswa kujiandaa mapema.

Maana kila kiongozi hupenda awe na watu wa namna yake anayoipenda yeye, unaweza kuwa ulikuwa mtendaji mzuri sana wa kazi, akaja kiongozi ambaye hatakutambua utendaji wako wa kazi.

Hili tunajifunza kwa Yusuf, tunafahamu sifa nyingi za Yusuf alipokuwa utumwani Misri, Farao alimpa nafasi ya juu sana. Lakini alivyokuja mfalme mwingine hakumjua Yusuf, ni kama haingii akilini ila ndio ukweli wenyewe.

Rejea: Basi akainuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu. Akawaambia watu wake, Angalieni, watu wa wana wa Israeli ni wengi tena wana nguvu kuliko sisi. KUT. 1:8‭-‬9 SUV.

Hapa unaweza kujitathimini mwenyewe maana ni mambo ambayo hutokea katika maisha yetu ya kila siku, ulikuwa una nafasi fulani lakini alivyoingia madarakani kiongozi mwingine akabadilisha uongozi mzima.

Maisha ya wana wa Israel yalibadilika ghafla, vile walikuwa wanaishi maisha ya uhuru, hayo maisha yalibadilika ghafla baada ya ndugu yao Yusuf kutotambuliwa na uongozi mpya wa mfalme.

Rejea: Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi. KUT. 1:11 SUV.

Yale maisha waliyozoea kuishi yakageuka maisha ya uchungu, ni kama wamisri walikuwa wanasubiri hiyo nafasi ya kuwatumikisha wana wa Israel ifike.

Rejea: Wamisri wakawatumikisha wana wa Israeli kwa ukali; wakafanya maisha yao kuwa uchungu kwa kazi ngumu; kazi ya chokaa na ya matofali, na kila namna ya kazi ya mashamba; kwa kazi zao zote walizowatumikisha kwa ukali. KUT. 1:13‭-‬14 SUV.

Hili linaweza kutokea kwa mtu yeyote hasa yule ambaye yupo kwenye nafasi ya uongozi, unaweza ukawa uongozi wa kanisa au unaweza ukawa uongozi wa serikali.

Kumbuka hili siku zote, ni ngumu sana kukubalika na uongozi wa awamu mbili tofauti, unaweza ukakubalika sana katika utendaji wako wa kazi nzuri kwa uongozi wa sasa. Lakini usikubalike na uongozi mwingine mpya utakaoingia, sio kana kwamba kiwango chako cha utendaji umeshuka, hapana.

Hii ikusaidie kujiweka vizuri, usiwe na kiburi na kujiona umefika, kumbuka huo uongozi au utawala una mwisho wake, na mwisho ukifika utawala mwingine ukaingia usishangae ukapoteza nafasi yako ya kazi.

Maarifa haya tunayapata kupitia usomaji wa Neno la Mungu, vizuri ukajenga tabia ya kusoma Biblia yako na kutafakari yale unayosoma. Kufanya hivyo kutakufanya ufunguke maeneo mengi sana katika maisha yako ya kimwili na kiroho.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081