Haleluya, ninakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, habari za wakati huu ndugu yangu. Bila shaka unaendelea kumtafakari na kumtukuza Mungu ndani ya moyo wako, kwa matendo yake makuu juu ya maisha yako. Usije ukaruhusu jambo lolote lile linaloujeruhi moyo wako, likakurudisha nyuma na ukaachana na safari uliyoanza nayo, epuka sana hilo.

Tunapooka tunakuwa tunajua tulipotoka, na tulipo sasa, na ili wokovu wetu usiwe na dosari wala maswali. Tunapaswa kuanza kujitofautisha kabla ya kuokoka na baada ya kuokoka. Kama zamani za ujinga tulikuwa watu wanaopenda kuketi baa na marafiki zetu tukinywa pombe, ukishaokoka hupaswi kuambatana na marafiki hao ukijifariji wewe hunywi ila utakuwa unakunywa tu soda.
Kufanya hivyo pasipo kujijua mwenyewe, utajikuta umerudia mtindo uleule wa unywaji wako wa pombe.

Tunapokuwa tumeamua kuokoka na kuachana na *UASHERATI/UZINZI*, tunapaswa kujitenga na mazingira yaliyokuwa yanatupelekea sisi kuwa katika uchafu ule. Huwezi kusema umeacha uzinzi/uasherati, wakati bado unaendeleza mawasiliano yasiyofaa na watu wako walewale wa zamani. Unakuta sms za mapenzi mapenzi tu wakati hao wadada/wakaka au wamama/wababa ulishaamua kuachana nao, na uliamua kuanza maisha mapya ya wokovu.

Sijakuambia uanze kutukanana nao, sijakuambia uanzishe ugomvi nao, nakueleza habari za kuendeleza mawasiliano nao. Kwa sababu unapoanza maisha ya WOKOVU, utakuwa na kiwango kidogo sana cha kuweza kukabiliana na mambo magumu ya kukuepusha na hali ya kutorudia ya nyuma.

Huwezi kusema umeokoka, alafu bado simu/tablet/laptop yako imejaza picha za ngono, umezifungia na password kabisa ili watu wasiweze kuziona kwa uharaka. Hapo unasema umeokoka ila kuna vitu bado huwezi kuvifuta katika kumbukumbu zako.

Unasema umeokoka alafu bado unaendeleza tabia ile ile ya kuwafolenisha/kuwapanga wadada wengi na kuwajaza maneno ya utawaoa. Kumbe ndani yako unajua kabisa unawadanganya, na unajua kabisa huwezi kuwaoa wote watano.

Unasema umeokoka dada alafu ile tabia yako ya zamani kabla hujaokoka bado unaiendeleza. Yaani umewapanga wanaume kama sita hivi, alafu wote umewapa majibu ya ndio nitaolewa na wewe. Mbaya zaidi unawatumia wanaume wale kwa matumizi yako ya kila siku, umewapanga kwa mafungu; huyu wa vocha, huyu wa saloon, huyu wa bajaji/bodaboda, huyu wa matumizi madogodogo ya chuo, huyu wa kodi ya nyumba, na huyu mwingine hana anachotoa na ndio tengemeo lako la kuishi naye.

Hapo unajiita umeokoka na umeachana na ya kale, ndio kwa viwango hivyo yaani! umeshindwa kuelewa wokovu unahitaji kuingia mzima mzima. Huhitaji kubakisha mguu mmoja nje na mguu mwingine ndani, yote inapaswa kuwa ndani.

Lakini tunasoma habari za Asa, baada ya kuachiwa kiti na baba yake Abiya. Asa akaondoa miungu yote ya kigeni iliyokuwepo, na kuwaambia watu wake wote wamwabudu Mungu wa kweli. Na Mungu akawapa kustarehe kwa kipindi kirefu cha uongozi wake Asa.

REJEA: Basi, Asa akafanya yaliyo mema, yaliyo ya adili, machoni pa BWANA, Mungu wake; maana aliziondoa madhabahu za kigeni, na mahali pa juu, akazivunja nguzo, akayakata-kata maashera; akawaamuru Yuda wamtafute BWANA, Mungu wa baba zao, na kuzitenda torati na amri. Tena akaondoa kutoka miji yote ya Yuda mahali pa juu na sanamu za jua; ufalme ukastarehe mbele yake. 2 NYA. 14:2‭-‬5 SUV.

Unapoamua kumfuata Yesu Kristo, amua kweli kuondoa tabia ambazo ulikuwa nazo kabla hujamjua Kristo. Ondokana kabisa na vijitabia ambavyo unaona vinakurudisha nyuma kiroho, vitabia ambavyo unaona vinaondoa uhusiano wako na Mungu.

Usiishi kama mwana aliyefungwa wakati haupo tena utumwani, ishi kama mwana aliye kwa baba yake. Jitofautishe kabla hujaokoka na baada ya kuokoka, ili hata wale ulioachana nao katika dhambi wamshuhudie kweli YESU wako.

Mungu akubariki sana, nakushukuru sana kwa muda wako, endelea kutafakari zaidi.

Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
+255759808081.
chapeo@chapeotz.com