“Yesu akamwambia, Ukiweza! Yote yawezekana kwake aaminiye”, Mk 9:23 SUV.

Swali hili linaweza kukushangaza na kufikiri huenda limekosewa kuulizwa, ni kuhakikishie kuwa halijakosewa, bali lipo sahihi kabisa.

Kauli hii tumeitumia sana tulio wengi kuwa mambo yote yanawezekana kwake Yesu, na tumekiri wazi kuwa kila tuombacho kwake kinawezekana kuwa vile tumeomba kwake.

Siwezi kuwa kinyume na hili ila napenda utafakari vizuri, kweli mambo yote tunayoomba kwa Mungu huwa yanatokea kama tulivyoomba? Bila shaka sio yote uliyowahi kuomba ulijibiwa kama ulivyoomba.

Kauli hii ya Yesu “yote yanawezekana” haipaswi kuchukuliwa kama ahadi isiyokuwa na masharti yeyote kwa mwombaji.

Neno “yote” unapaswa kulielewa kuwa halimaanishi kila kitu tunachoweza kufikiri kumwomba Mungu kitakuwa vile tuliomba. Maombi ya Imani ni lazima yajengwa juu ya mapenzi ya Mungu, kumbuka hili siku zote za maisha yako.

Fahamu kwamba hatuombi kitu chochote cha kipumbavu au cha kipuuzi au kibaya kwa kigezo kuwa yote tuombayo yanawezekana kwake.

“Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu”, Yak 4:3 SUV.

Imani inayotakiwa kwa mwamini lazima ipokelewe kama karama ya Mungu, Mungu mwenyewe huipandikiza ndani ya moyo wa yule mtu aitafutaye kwa bidii zote.

Mtu yule anayeishi kwa uaminifu sawasawa na mapenzi ya Mungu yanavyomtaka, yule anayeenenda katika njia zinazompendeza Mungu wao.

Mtu anayeenenda vyema mbele za Bwana, mtu anayejua kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu, na mwenye Imani thabiti, mtu huyo anaweza kuomba chochote na Mungu akatenda kwake.

“Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu”, Mt 17:20 SUV.

Tusiwe na dhana ya kuwa kila jambo na kila mtu atakayeomba kwa Mungu lolote litawezekana, yapo mambo tutayaomba nje na mapenzi ya Mungu, tuwe na uhakika mambo hayo hayatakuwa kama tulivyoomba.

Tuwe na mahusiano mazuri na tunayetaka kumwomba, na tujue mapenzi yake ni yapi, ili tusije tukaomba vitu vilivyo nje na mapenzi yake kwa kigezo kuwa yote yanawezekana kwake.

Soma neno ukue kiroho
Mungu akubariki sana
Samson Ernest