Siku moja nikamsikia mtu mmoja anasema akifika peponi ataoa mke mzuri, ni kama jambo la kushangaza kumsikia mtu akizungumza maneno kama hayo. Ila mtu huyu ndio anaamini hivyo, amejengwa katika msingi wa namna hiyo.

Haijalishi una mke mzuri sana hapa Duniani, jua huyo ni wa hapa hapa Duniani, wala haijalishi una mume mzuri sana na unampenda sana. Mpende sana ukiwa Duniani, mbinguni hakuna kuishi na mume wako, huko ni habari nyingine kabisa.

Usije ukawa unajijaza ujinga kuwa mke/mume wako akifa mtaenda kuoana huko mbinguni, alafu mnaendeleza uhusiano wenu wa ndoa au ukawa unafikiri utaenda kuoa mke mwingine au utaenda kuolewa na mwanaume mwingine. Fahamu mbinguni hakuna kuoa wala kuolewa.

Haijalishi umepewa elimu ya namna gani inayohusu kuishi na mume/mke wako huko mbinguni/peponi, elewa huo ni uongo. Mbinguni kazi yetu itakuwa kumsifu Mungu, hakuna habari za kuoa/kuolewa.

Rejea: Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa mke, akafa hana mtoto; na wa pili [akamtwaa yule mke, akafa hana mtoto;] hata wa tatu akamwoa, na kadhalika wote saba, wakafa, wasiache watoto. Mwisho akafa yule mke naye. Basi, katika ufufuo atakuwa mke wa yupi? Maana aliolewa na wote saba. Yesu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi. LK. 20:29‭-‬35 SUV.

Tena mbinguni hakuna kufa, wala hakuna kuugua, tutabaki tulivyo na miili yetu mipya tutakayoivalisha siku ya unyakuo. Hii sio ya kukosa ukiwa kama mkristo ambaye una kiu ya kwenda kuishi maisha ya umilele.

Haijalishi ulikuwa unajua miaka mingi kuwa mbinguni tunaenda kuoa/kuolewa, achana kabisa na imani hiyo potofu. Mbinguni hatufanyi hayo mambo, acha kujidanganya kutokana na mafundisho ya uongo uliyonayo moyoni.

MUHIMU; Je, Unapenda kukua kiroho kwa kusoma Neno la Mungu kila siku bila kuishia njiani? Chapeo Ya Wokovu whatsApp group ni jibu lako, tuma ujumbe wako whatsApp kwenda +255759808081 ili uunganishwe kwenye group hili lenye nidhamu nzuri sana.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
+255759808081