“Basi, katika kiyama atakuwa mke wa yupi katika hao? Maana wote saba walikuwa naye”, Mk 12:23 SUV.

Zipo dhana nyingi sana juu ya hili, wapo wanaamini kuwa tukifika mbinguni tutaoa na wengine kuolewa.

Wapo wamebaki njia panda, ipi ni sahihi, na ipi sio sahihi, kutokana na mkanganyiko wa mafundisho mbalimbali tofauti juu ya hili.

Sio vibaya kunitiana moyo kuwa ukifiwa na mwenza wako kuna maisha mengine, na mtaenda kukutana na  kuoana tena. Ujue huko ni kudanganyana.

“Yesu akajibu, akawaambia, Je! Hampotei kwa sababu hii, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu? Kwa maana watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika walioko mbinguni” Mk 12:24‭-‬25 SUV.

Mafundisho haya ya Yesu hayamaanishi kuwa mume na mke hawataweza kufahamiana au hawatatambuana kabisa kwa sura wakifika mbinguni.

Wakati tutapofika mbinguni uhusiano wetu na wenzi wetu tukiwa hapa duniani, utakuwa wa kina zaidi hasa kiroho.

Ingawa hautawaliwa na muunganiko wa ndoa kama ilivyo sasa tukiwa hapa duniani, na tukiwa tunaishi pamoja kama wanandoa wanaopendana.

Inawezekana unampenda sana mke au mume wako, ujue ndoa yenu itaishia pale mmojawapo atapofariki au kunyakuliwa.

Siku mtapofariki wote hakutakuwepo na maisha mengine ya ndoa kama mlivyokuwa duniani, hili unapaswa kulifahamu.

Ikiwa una dhana kuwa mbinguni au wengine huita peponi, kutakuwa na kuoa na kuolewa, tutapata waume au wake wazuri wa sura na wanaotupenda, tutakuwa tunajidanganya.

Ninao ujasiri wa kusema hivi kwa sababu Yesu alishamaliza utata huu, aliweka wazi kabisa kuwa hakuna kuoa wala kuolewa.

Mthamini na kumjali mwezi wako mkiwa hapa duniani, mbinguni tutakuwa na maisha mengine kabisa mapya. Wala hakutakuwepo na kuoa na kuolewa.

Soma neno ukue kiroho
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081