Hili sio jambo geni katika masikio yetu, Mara nyingi tumeona mtu fulani akiwa na utiisho fulani na kuhofiwa sana na watu.

Huenda kuwa tumekuwa na maswali ambayo hayana majibu, ama huenda tumekuwa na majibu yasiyo sahihi kwa huyo mtu.

Anaweza akawa kiongozi kabisa ila akawa na utiisho mkubwa na kujenga hofu kwa watu, hii kwa upande mwingine wapo wanaoona ni vizuri watu kuwa na hofu nao.

Wasiojua anayetoa utiisho huu ni nani, na wasiomjua Kristo, unaweza ukawakuta wametumia njia zisizo halali/nzuri kuutafuta huo utiisho mkubwa kwa watu.

Asili ya hili la utiisho na kuhofiwa na watu, au wale unaowaongoza ni jambo ambalo linatoka kwa Mungu mwenyewe.

Kwahiyo utiisho na kuhofiwa na watu wengine, hili linawekwa kwa mtu na Mungu mwenyewe kwa kazi maalum ambayo anayo huyo aliyepewa

Hili jambo tunaliona katika maandiko matakatifu, ahadi moja wapo ya Mungu kwa wana wa Israel ilikuwa kuwapa utiisho na kuhofiwa na watu wa nchi ile ambayo Bwana aliwaahidia kuwapa, na mahali popote watakapokanyaga.

Rejea: Hapatakuwa na mtu atakayeweza kusimama mbele yenu; BWANA, Mungu wenu, ataweka utisho wenu na kuhofiwa kwenu juu ya nchi yote mtakayoikanyaga, kama alivyowaambia. KUM. 11:25 SUV.

Unaweza kuona ni jinsi gani Mungu mwenyewe ndio mtoa utiisho na kuhofiwa na watu, sasa wengine wasiojua hili huwa wanakimbilia kusema anatumia nguvu za giza.

Inawezekana kabisa akatumia njia zisizo halali kama nilivyotangulia kusema hapo awali, lakini jambo la kuzingatia hapa ni kwamba asili ya hili ni kutoka kwa Mungu mwenyewe.

Mungu tangu mwanzo aliwaahidi wana wa Israel kuwapa utiisho, kwahiyo mwenye kuweza kutoa utiisho wa kweli na ukawafanya maadui zako wakakukimbia ni Mungu mwenyewe.

Rejea: Nitatuma utisho wangu utangulie mbele yako, nami nitawafadhaisha watu wote utakaowafikilia, nami nitawafanya hao adui zako wote wakuonyeshe maungo yao. KUT. 23:27 SUV.

Ukiona mtumishi wa Mungu ana utiisho fulani mkubwa, ujue ni Mungu mwenyewe amempa huo utiisho kwa kazi yake maalum.

Utiisho na kuhofiwa na watu kunatoka kwa Mungu mwenyewe, kama unatamani hichi kitu kiwe kwako. Kama unataka uutumie huu utiisho kwenye nafasi ya uongozi uliyonayo, inawezekana ukawa nao.

Cha kufanya ni kumpokea Bwana Yesu moyoni mwako, na kuishi maisha matakatifu, maisha yanayompendeza Mungu.

Na uwe unatambua hii ahadi ni ya Mungu mwenyewe, itakuwa rahisi kwako kuidai kwa Mungu kama hutaiona ikitenda kazi kwako.

Hatuombi tuwe na utiisho mkubwa na kutia watu hofu ili tuwe shida kwa watu, utiisho huu una kazi yake maalum ambayo Mungu anawapa walio wake kuwasaidia.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com