Unaweza kujitahidi kusoma Neno la Mungu kwa wingi, unaweza kujitahidi kusikiliza sana mafundisho ya Neno la Mungu. Lakini kama hutoweka katika matendo yale unayojifunza, haitokuwa na maana yeyote ya kujifunza kwako Neno la Mungu.

Kujifunza Neno la Mungu kunahitaji kulipeleka katika matendo, kile unajifunza ndani ya biblia unapaswa kuwa na muda wa kuyaweka kwenye matendo yale unayojifunza.

Maeneo yafuatayo yanaweza kutusaidia kujitambua/kujijua tupo kwenye kundi gani katika kujifunza/kulisoma Neno la Mungu na kulitendea kazi;

1. Kando Ya Njia; ni mtu aliyesoma vizuri Neno la Mungu, na kuona linaweza kumsaidia kabisa katika maisha yake. Baada ya kusikia tu, na kabla hajaanza kulitendea kazi, Shetani huja na kuliondoa hilo Neno moyoni mwake.

Anapoondolewa hilo Neno moyoni mwake ile hatua aliyojiandaa kuichukua, inakuwa imepotezwa kwa njia hiyo. Kama alikuwa amejipanga leo, kesho utamwona amepoa kama sio yule wa jana aliyekuwa ameweka mikakati mizuri ya kulifanyia kazi Neno la Mungu.

Rejea: Hawa ndio walio kando ya njia lipandwapo neno; nao, wakiisha kusikia, mara huja Shetani, akaliondoa lile neno lililopandwa mioyoni mwao. Marko 4:15.

2. Penye Miamba; ni wale watu wanalisoma Neno la Mungu na kulipokea kwa furaha/shangwe kubwa, na ni wale watu wanaojifunza Neno la Mungu kupitia kwa watumishi mbalimbali wa Mungu.

Wanaposoma au wanapojifunza huwa wanalipokea kwa furaha kubwa sana, ila ndani yao kunakuwa hakuna mizizi. Na unajua mti usipokuwa na mizizi imara iliyojichimbia chini vizuri mwisho wake huangushwa na upepo mkali unapokuja.

Pale inapokea misukosuko ya Dunia hii, pale changamoto ngumu za maisha zinapomkuta mkristo, hushindwa kuzihimili hizo changamoto ngumu na hujikuta wakianguka dhambini.

Mfano inaweza ikawa shida ya pesa, kama ni mwanafunzi anaweza kuanguka kwenye uasherati kwa sababu aliyetoa msaada alimpa sharti la kulala naye kimapenzi.

Kwa kuwa hakuwa na Neno lenye mizizi imara ndani yake, akajikuta anaingia kwenye mtego mbovu ambao alikuwa na uwezo wa kuwepuka huo mtego.

Rejea: Kadhalika na hawa ndio wapandwao penye miamba, ambao kwamba wakiisha kulisikia lile neno, mara hulipokea kwa furaha; ila hawana mizizi ndani yao, bali hudumu muda mchache; kisha ikitokea dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara hujikwaa. Marko 4 :16-17.

3. Penye miiba; ni wale watu wanaojifunza vizuri Neno la Mungu lakini shughuli za Dunia hii huwasonga sana mpaka lile Neno walilojifunza linakosa nguvu ya kutenda kazi ndani yao.

Wengine udanganyifu wa mali walizonazo huwafanya walipuuze Neno la Mungu walilolisoma vizuri, kwa kuona halina uzito sana. Maana wengine huona linawabana sana, hasa kwenye kujichumia mali zisizo halali.

Kwahiyo Neno la Mungu linaposongwa na miiba mingi, hilo Neno halitaweza kuzaa matunda mazuri kwa huyo mtu hata kama lipo kwenye udongo mzuri. Maana limesongwa na miiba ya kutosha.

Rejea: Na hawa ndio wale wapandwao penye miiba; ni watu walisikiao lile neno, na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile neno, likawa halizai. Marko 4 :18-19.

4. Penye udongo mzuri; ni wale watu wanalisoma Neno la Mungu, na wanaolisikia Neno la Mungu kupitia kwa watumishi wa Mungu. Alafu hilo Neno la Mungu hulipokea na kulitendea kazi vile linamwelekeza afanye.

Kama Neno la Mungu limemwambia acha kuabudu sanamu ni chukizo kwa Mungu, hataishia kusoma tu, atachukua hatua ya kuachana na habari ya kuabudu sanamu.

Kama alikuwa ana chuki na watu, alikuwa hana tabia ya kusamehe wale waliomkosea, akakutana na Neno la Mungu linamtaka asamehe wale waliomkosea. Lazima atachukua hatua ya kuachana na chuki, na kuwa na moyo wa kusemehe.

Watu wa namna hii huzaa matunda mengi sana mazuri kadri wanavyozidi kulijua Neno la Mungu, watu wa namna hiyo huwa hawachoki njiani kuhusu kusoma Neno la Mungu.

Rejea: Na hawa ndio waliopandwa penye udongo ulio mzuri; ni watu walisikiao lile neno na kulipokea, na kuzaa matunda, mmoja thelathini, mmoja sitini, na mmoja mia. Marko 4 :20.

Upo kundi namba ngapi kati ya hayo? Nakushauri uwe kundi la mbegu namba nne, mbegu iliyopandwa penye udongo mzuri ikaota na kuzaa matunda mazuri. Utaliona Neno la Mungu lina msaada mkubwa sana katika maisha yako.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com