
Ni swali ambalo limekuwa likiwasumbua watu wengi, hasa pale mtu anapookoka, anaanza kuona mke/mume aliyekuwa naye kabla ya kuokoka anapaswa kumwacha/kuachana naye.
Wakati anawaza kumwacha mwenzake, mwenzake anakuwa yupo tayari kuendelea kuishi naye kama mume na mke, lakini changamoto inakuwa kwa mmoja wapo aliyeokoka.
Hili jambo tunapaswa kuwa nalo makini sana, hasa wale wanaokoka wakiwa tayari walishaolewa au walishaoa, kama mke wako anapenda kuendelea kuishi na wewe baada ya kuokoka hupaswi kumwacha.
Na kama mume wako anakubali kuendelea kuishi na wewe baada ya kuokoka, hupaswi kumwacha ukaenda kuolewa na mwanaume mwingine aliyeokoka. Kwa kisingizio cha kuwa huwezi kuishi na mwanaume ambaye hajaokoka.
Rejea: Lakini watu wengine nawaambia mimi, wala si Bwana, ya kwamba iwapo ndugu mmoja ana mke asiyeamini, na mke huyo anakubali kukaa naye asimwache. Na mwanamke, ambaye ana mume asiyeamini, na mume huyo anakubali kukaa naye, asimwache mumewe. 1 KOR. 7:12-13 SUV.
Umeona hapo ndugu, kama mume wako anakubali kuendelea kuishi na wewe baada ya kuokoka, huna haja ya kumkimbia, na kama mke wako anakubali kuendelea kuishi na wewe baada ya kuokoka vizuri ukaendelea naye.
Hawa ni watu ambao walikuwa hajampokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yao, inawezekana walikuwa watu wa dini tu. Ila walikuwa ni watu wanaomkataa kabisa Yesu Kristo ila siku ikafika mmoja wapo akakubali kumpokea Yesu Kristo, wanaruhusiwa kuendelea kuishi pamoja.
Hakuna anayewazuia, wala hakuna mwenye mamlaka ya kuwatenganisha kama wote wanapendana, hata kama mmoja wapo ameokoka, na bado wanaendelea kuonekana wapo kitu kimoja. Hawapaswi kuachana.
Kupitia mmoja wapo aliyeokoka sawasawa, anaweza akawa chachu ya kumfanya mwenzake aokoke, mwisho wanakuwa watu wanaomjua Kristo wote.
Rejea: Kwa maana wajuaje, wewe mwanamke, kama utamwokoa mumeo? Au wajuaje, wewe mwanamume, kama utamwokoa mkeo? 1 KOR. 7:16 SUV.
Kama itatokea mmoja wapo hataki kukaa na mwenzake baada ya kuokoka anaruhusiwa kuondoka, na huyu aliyeokoka/aliyeamini alafu akaachwa anaruhusiwa kuoa/kuolewa na mtu mwingine.
Rejea: Lakini yule asiyeamini akiondoka, na aondoke. Hapo huyo ndugu mume au ndugu mke hafungiki. Lakini Mungu ametuita katika amani. 1 KOR. 7:15 SUV.
Unaona hapo, kama asiyeamini/asiyeokoka akiondoka, huyu ndugu aliyeokoka na aliyeachwa anaruhusiwa kuoa/kuolewa. Maana hafungwi tena, baada ya mwenzake kumwacha akaenda zake.
Maandiko yapo wazi, haya ndio yanatusaidia kuondoa maswali mengi ambayo mengine huwa yanatufanya tubaki njia panda. Lakini tunapoyasoma na kuyaelewa tunakuwa tumefahamu njia ipi ni sahihi kuifuata.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com