
“Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi?” Mt 6:25 SUV.
Hebu tuliangalie hili jambo, je tunapaswa tu kuwa bize na mambo ya Mungu na kuacha mambo mengine yanayohusu kazi zetu za mikono? Yaani badala ya kutumia muda mwingi kwenye kazi maofisini au mashambani tuwe bize na kuhubiri injili tu?
Yesu haaminishi kwamba ni vibaya kujishughulisha kwa ajili ya mahitaji ya kimwili ya kujipatia kipato chetu cha kila siku na kujiwekea akiba za siku za baadaye.
Familia yako au watoto wako wanapaswa kutunzwa na mzazi wao, sio unawaacha watoto wako wanalala njaa alafu wewe upo bize kuhubiri injili, au kuzunguka huku na kule alafu watoto wanakosa mahitaji yao ya msingi.
“Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini”, 1 Tim 5:8 SUV
Ikiwa ni hivi maana yake unapaswa kuhakikisha watoto wako wanakula na kusoma vizuri, ikiwa ni mke unapaswa kuhakikisha mke wako anapata mahitaji yake, usitekeleze familia yako ukawa bize na huduma. Huku ukijifariji na maneno haya;
“Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao?” Mt 6:26 SUV
Ukifanya hivyo ujue una shida katika ukristo wako, ujue unajitafutia laana zisizo na sababu kwa kutafasiri maandiko vibaya, utasema shida ipo wapi mbona napambana kuhubiri mtaa kwa mtaa, kijiji kwa kijiji, sawa haina shida, unajua familia yako inakula nini?
Lazima ujue hilo, ikiwezekana weka mazingira vizuri, lima uwe na chakula cha kutosha, tafuta kibarua ufanye upate pesa ya kula na watoto wako, hii ndio akili za watoto wa Mungu. Hatuokoki tuwe wajinga, na hicho unapokipata kwenye huduma, labda umepata posho, moyo wako uwe kwa familia yako, usile peke yako ukawaacha watoto wako.
Yesu alikuwa na maana gani sasa kusema maneno haya; “Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini”… Mt 6:25 SUV.
Jambo analolikataza Yesu ni wasiwasi au hofu inayoonesha upungufu wa Imani katika uangalizi na upendo wa kibaba wa Mungu.
“Huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu”, 1 Pet 5:7 SUV.
Pale tunapowajibika katika nafasi zetu, kufanya kazi kwa bidii, lakini tukawa hatujapata kama tulivyotarajia, tusiwaze kupita kiasi, tusiwe na hofu itakuwaje kesho, mwaka huu tutavukaje, maswali kama haya ni ya mtu aliyekosa tumaini kabisa.
Mungu wetu hujishughulisha na mambo yetu, tunapaswa kumwendea yeye kumweleza shida zetu na mahitaji yetu, tukiamini yeye ndiye atupaye mahitaji yetu.
Na kipaumbe chako kisije kikawa kupambana kuhangaikia mambo ya mwili tu, hakikisha kipaumbele chako kinakuwa kwa mambo ya Mungu, fanya mambo yote ila Mungu awe wa kwanza katika maisha yako.
Soma neno ukue kiroho
Mungu akubariki sana
Samson Ernest
+255759808081