Tunaweza tukawa mafundi wa kuongea sana na kulalamika sana juu ya jambo fulani ambalo haliendi sawa. Kulalamika kwetu kunaweza kusiwe na kumhusisha Mungu wetu hata kidogo.

Mtu analalamika ndoa yake inamsumbua, muulize ameenda mbele za Mungu mara ngapi kuombea ndoa yake. Muulize huyo mume wake anayemlalamikia, amemweleza Mungu? Muulize huyo mke wake anayemsumbua ameenda mbele za Mungu kumweleza/kumlilia?

Utakuta hakuna hatua yeyote aliyochukua, kama ni maombi ni yale ya kuombea chakula, yaani maombi ya dakika mbili. Maombi ambayo hayana uzito wowote mbele za Mungu, hata moyoni mwake haoni kama ameomba.

Tunalalamika mambo yamekuwa magumu, umewahi kutenga muda wako hata wa lisaa limoja kwa ajili ya kuombea taifa lako? Unaweza ukawa hujawahi kufanya hivyo, hayo ni maombi ya kawaida kabisa ukiwa umeshiba chakula chako kizuri.

Jiulize ni lini umeacha kula kwa ajili ya kuombea taifa lako, kwa ajili ya kuombea ujana wako, kwa ajili ya kuombea uchumba wako, kwa ajili ya kuombea harusi yako, kwa ajili ya kuombea ndoa yako, kwa ajili ya kuombea biashara zako, na kwa ajili ya kuombea kazi yako na nk.

Unaweza kuta hujawahi kufanya hilo zoezi hata siku moja, umekuwa mtu wa malalamiko tu ya mdomoni. Malalamiko ambayo hayamhusishi Mungu chochote, hakuna siku umetenga muda maalum wa kumwomba Mungu akusaidie.

Utasemaje Mungu hakusaidii, utasemaje kitu ambacho hujaenda mbele za Mungu kutafuta msaada wake. Huwezi kulalamika ila kwa sababu Mungu amekupa Neema ya kuwa na mdomo, utaongea utakavyoweza.

Hebu tuangalia Neno la Mungu linatuambia nini katika haya, huenda unashindwa kunielewa vizuri ninachosema hapa, na huenda unafikiri naongea mambo ambayo hayapo kimaandiko.

Rejea: Inuka, ulalamike usiku, Mwanzo wa makesha yake; Mimina moyo wako kama maji usoni pa Bwana; Umwinulie mikono yako; Kwa uhai wa watoto wako wachanga wazimiao kwa njaa, Mwanzo wa kila njia kuu. OMB. 2:19 SUV.

Inuka mlilie Mungu wako juu ya watoto wako wanaokusumbua, inuka umlilie Mungu wako juu ya watoto wanaokosa chakula, inuka umlilie Mungu juu ya familia yako. Kama familia yako ina amani, zipo familia za marafiki zako zinapitia wakati mgumu na wewe unaona hilo, inuka umlilie Mungu wako.

Lalamika mbele za Mungu, chukulia uzito wa jambo unalopeleka mbele Mungu. Nenda mbele Mungu ukiwa umejiandaa, ukienda mbele za Mungu bila kujiandaa ndio yale ya kusinzia kwenye maombi.

Mtu unaingia kwenye maombi huna hata nusu saa usingizi unakushika, hayo sio maombi ya mtu anayemaanisha. Mtu anayemaanisha hawezi kusinzia kwenye maombi, labda pawepo na tatizo lingine.

Acha kuumia tu juu ya jambo fulani ambalo unaona halipo sawa, nenda mbele za Mungu, omba maombi yanayoeleweka. Sema na Mungu wako kama unasema na rafiki yako wa karibu sana unayejua shida uliyonayo, yeye anaweza kuitatua shida yako na si mwingine.

Usikae unalalamika mimi siolewi, umechukua hatua gani mbele za Mungu, umetenga hata siku mbili ya maombi ya kujinyima kula? Kuonyesha unyenyekevu mbele za Mungu, kuonyesha usiriazi wa hitaji lako, umewahi kufanya hivyo?

Na kama umewahi ni mara ngapi umefanya hivyo, au ulivyofanya mara moja ulivyoona hujibiwi maombi yako. Ukaacha na kuomba, kama uliacha kuomba, uache na kulalamika, neno la Mungu linasema “ombeni bila kukoma”.1 THE. 5:17 SUV.

Hebu tujifunze kwenda mbele za Mungu kwa maombi yetu, tuache maneno mengi yasiyo na msingi wowote. Umeona jambo ni nzito na ukiliangalia unaona unaenda kuzama, piga magoti omba Mungu haswa, acha kulialia ovyo huku huombi.

Unajua mwenyewe unayopitia, katika hayo unayopitia umemkabidhi Mungu ashughulike nayo? Yaani umeenda mbele za Mungu kwa machozi juu ya hilo linakusibu? Kama ni hapana nakuomba uache kuongea badala yake ingia katika maombi.

Mungu atusaidie sana tuwe waombaji.
Chapeo Ya Wokovu.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.